Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) limetoa ufafanuzi kuhusu madai ya klabu ya Yanga sc kuhusiana na fedha za zawadi ya ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB kwa msimu uliopita.
TFF imelazimika kutoa taarifa hiyo kutokana na madai ya klabu ya Yanga sc kupitia msemaji wao Ally Kamwe aliyedai kuwa klabu hiyo haijalipwa fedha zake za ubingwa wa Kombe la shirikisho kwa miaka mitatu mfululizo.
“Tumemsikia meneja wa habari na mawasiliano wa Yanga sc kupitia vyombo vya habari akidai kuwa klabu yao inaidai TFF shilingi milioni 200, ambayo ni zawadi ya ubingwa wa Kombe la shirikisho la benki ya CRDB,” imeeleza taarifa ya TFF.
Hata hivyo, TFF imefafanua kuwa hali ni tofauti, na kwamba klabu hiyo ndiyo inadaiwa na TFF na wamewataka wahusika kuwasili klabuni hapo mapema hii leo ili kuhakiki madeni yao.
“Tungependa kuweka bayana kuwa TFF ndiyo inayoidai klabu hiyo kwa kuwa Yanga sc iliwasilisha barua ikiomba fedha zao za zawadi kutoka mashindano mbalimbali zitumike kulipia madeni yao kwa TFF, ikiwemo ada za wachezaji wa kigeni”, imeeleza taarifa hiyo.
TFF imesisitiza kuwa, ili kuondoa mkanganyiko kwa umma, tayari imeshaiandikia Yanga barua ikiitaka kutuma mtaalamu wao wa fedha siku ya Juni 11 saa 4:00 asubuhi kwa ajili ya kuhakiki deni hilo akiwa na vielelezo vyote, katika ofisi za Shirikisho hilo.