Katika ramani ya michezo Barani Afrika, Tanzania imebahatika kuwa na Uwanja wa kihistoria na wa kisasa unaosimama kama fahari ya jiji la Dar es Salaam .
Fahari hii si nyingine bali ni Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo eneo la Uhuru, Temeke, ni sehemu ambayo kila shabiki wa michezo nchini hupata fahari kubwa kila anaposimama kuangalia uwanja huu wenye uwezo wa kubeba zaidi ya watazamaji 60,000 kwa wakati mmoja. Ni kiwanja ambacho si tu kimekuwa alama ya michezo, bali pia sehemu ya kutangaza sura mpya ya taifa kwenye ramani ya Afrika na dunia.
Muundo na Ubora wa Uwanja
Ukisimama ndani ya uwanja wa Benjamin Mkapa, jambo la kwanza litakalokushangaza ni uzuri na ukubwa wake. Viti vyake vya rangi tofauti vinavyopangwa kwa umaridadi vinaunda mandhari yenye kuvutia kwa macho ya mashabiki na wachezaji. Mbali na kuwa na mfumo wa taa za kisasa zinazoweza kuangaza mechi hata usiku, uwanja huu pia umejengwa kwa viwango vya kimataifa, ukizingatia masharti ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na lile la Afrika (CAF). Nyasi zake za kijani kibichi, ambazo hupandwa na kutunzwa kwa umakini mkubwa, huwapa wachezaji urahisi wa kucheza mpira wa kiwango cha juu.
Usalama wa Kutosha
Hali ya usalama pia imepewa kipaumbele. Uwanja una milango ya kuingilia na kutoka zaidi ya kumi na tano, kitu ambacho hurahisisha msongamano wa mashabiki. Zaidi ya hayo, kuna vyumba vya vyombo vya habari, vyumba vya wachezaji, na hata sehemu za wageni mashuhuri (VIP Lounge), jambo linaloufanya kuwa uwanja wa daraja la kwanza.
Michezo ya Kihistoria
Tangu kufunguliwa kwake mwaka 2007, uwanja huu umeshuhudia michezo mingi ya kuvutia ambayo imeandika historia kwenye kurasa za michezo nchini. Hakuna shabiki wa soka Tanzania asiyekumbuka mechi za watani wa jadi Simba na Yanga zinazovuta maelfu ya mashabiki na kufanya jiji la Dar es Salaam kusimama kwa muda. Hizi derby za Kariakoo, zikichezwa ndani ya Benjamin Mkapa, hujulikana kama “vita vya uswahilini” na mara zote hukonga nyoyo za mashabiki kutokana na burudani na msisimko unaoambatana nazo.
Mbali na michezo ya ndani, uwanja huu pia umekuwa mwenyeji wa mechi za kimataifa za timu ya taifa, Taifa Stars. Mechi nyingi za kufuzu Kombe la Dunia na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zimepigwa hapa, na mara kadhaa umati wa mashabiki umeushuhudia uwanja huu ukibadilika kuwa bahari ya rangi ya bendera ya taifa. Mechi ya kihistoria kati ya Taifa Stars na Uganda mwaka 2009, ambapo Stars walifanikiwa kufuzu kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya CHAN, bado inakumbukwa na mashabiki wengi.
Machinjio ya Vigogo Barani Afrika
Kama unaukumbuka ule msemo wa kwa “mkapa hatoki mtu” basi ni kuwa uwanja wa Benjamin Mkapa umewahi kushuhudia michezo ya kimataifa ya klabu ambapo vilabu vya Simba na Yanga wakiwa wenyeji,walifanikiwa kupindua meza kibabe kwa kupata ushindi uliowavusha kwenda hatua nyingine za michuano ya kimataifa licha ya kupoteza michezo ya awali ugenini.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Simba sc iliwahi kupindua meza kwa As Vita ya Congo,Nkana Red Devils ya Zambia na Al Masry ya Misri huku wakiwa wamewahi kuwapa vipigo wakali wa soka la Afrika kama Al Ahly, TP Mazembe, na Rs Berkane na wengine.
Pia Yanga sc nayo imewahi kuzipa vipigo timi za Tp Mazembe,Cr Belouizdad na wengine katika Mizunguko ya hatua ya makundi ya Caf.
Pia imeshuhudiwa michezo mbalimbali ya robo fainali na nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara kadhaa imepigwa hapa, na mara nyingi mashabiki hujitokeza kwa wingi kuhakikisha wapinzani wanakutana na “ukuta wa 12” wa mashabiki wa Tanzania.
Zaidi ya Soka
Ingawa mpira wa miguu ndio unaotawala zaidi, uwanja wa Benjamin Mkapa pia umetumika kwa shughuli nyingine za kijamii na kitaifa. Sherehe kubwa za kitaifa, matamasha ya muziki, na hafla za kidini mara kadhaa zimefanyika humo. Hii ni ishara kwamba uwanja huu ni sehemu ya maisha ya kila Mtanzania, si shabiki wa soka pekee.
Tegemeo la Afrika Mashariki na Kati
Klabu kadhaa Afrika Mashariki na kati mara kadhaa zimekua zikiomba kutumia uwanja wa Benjamin Mkapa kama uwaja wake wa nyumbani kutokana na nchi zao kutokua na viwanja vyenye hadhi ya Shirikisho la soka barani Afrika (Caf) au Shirikisho la soka Duniani (Fifa) hivyo zimekua zikiomba kutumia uwanja wa Benjamin mkapa kwa ngazi ya vilabu au timu zao za Taifa ambapo nchi kama Burundi na Sudan zimeshautumia uwanja huu kama uwanja wa nyumbani katika michezo yao.
Fahari ya Taifa
Kwa ujumla, uwanja wa Benjamin Mkapa ni alama ya maendeleo ya michezo nchini Tanzania. Ni sehemu ambayo inaleta watu pamoja – bila kujali rangi, dini, au kabila – kwa lengo moja la kufurahia michezo na burudani. Kwa uzuri wake, historia yake, na matukio makubwa yaliyoshuhudiwa humo, ni sahihi kusema kwamba uwanja huu ni almasi ya michezo ya Tanzania na fahari ya taifa.