Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limethibitisha kuufungulia rasmi Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi uliopo mkoani Tabora baada ya kukamilika kwa marekebisho muhimu ya miundombinu, hatua iliyoufanya uwanja huo kukidhi vigezo vya kikanuni na masharti ya leseni za klabu kwa mujibu wa sheria za mpira wa miguu.
Uwanja huo ulikuwa umefungiwa awali na TFF kutokana na kutokidhi masharti yaliyowekwa katika kanuni za Leseni za Klabu, hususan kwenye eneo la miundombinu ambayo ilionekana kuwa katika hali isiyoruhusu kuchezewa michezo ya mashindano ya kitaifa. Hata hivyo, baada ya uongozi wa uwanja huo kufanyia kazi maagizo ya TFF, shirikisho hilo limeufungulia rasmi uwanja huo kuendelea kutumika kwa michezo ya Ligi Tanzania Bara.
Taarifa iliyotolewa na TFF imeeleza kuwa timu ya ukaguzi ya shirikisho hilo ilifanya ziara ya ukaguzi wa miundombinu ya uwanja huo na kuridhishwa na maboresho yaliyofanyika kulingana na maagizo ya awali yaliyotolewa. Maboresho hayo yalihusisha sehemu ya vyumba vya kubadilishia nguo, eneo la kuchezea (pitch), majukwaa ya watazamaji, vyoo, na huduma zingine muhimu kwa mujibu wa viwango vinavyotakiwa.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
“Baada ya kukagua miundombinu ya uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, tumethibitisha kuwa marekebisho yaliyotakiwa yamefanyika kwa kiwango kinachokubalika. Hivyo, uwanja huo sasa umeidhinishwa rasmi kutumika kwa michezo ya Ligi,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya TFF.
Ufunguzi huu ni faraja kubwa kwa timu zinazotumia uwanja huo kama uwanja wa nyumbani, hasa klabu za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza, pamoja na mashabiki wa soka mkoani Tabora ambao sasa wataweza kushuhudia michezo ya ligi kwenye uwanja wao wa nyumbani. Hatua hii pia inatazamwa kama mafanikio ya juhudi za TFF kuhakikisha viwanja vinaboreshwa na vinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.