Baada ya kutangazwa kuachana rasmi na kocha Fadlu Davis pamoja na benchi lake la ufundi kwa makubaliano ya pande mbili, klabu ya Simba SC imeendelea kuwa gumzo katika mitaa ya soka nchini kutokana na kuhusishwa na makocha kadhaa mpaka sasa.
Habari zinazozagaa kwa sasa zinadai kuwa mabosi wa wekundu wa Msimbazi wapo mbioni kumshawishi kocha wa muda wa timu ya Taifa Stars, Hemed Suleiman Morocco, kuchukua mikoba ya Davis kwa muda, huku mchakato wa kumpata kocha mpya ukiendelea.
Kocha Hemed Morocco amekuwa akivutia macho mashabiki wengi kutokana na uwezo wake mkubwa aliouonyesha akiwa na kikosi cha Taifa Stars katika michuano ya CHAN na AFCON, ambapo licha ya changamoto alizokutana nazo, aliweza kuipa Stars mwonekano mpya wa kiuchezaji na kuamsha matumaini mapya kwa mashabiki wa soka la nyumbani.
Sifa hiyo imewafanya mabosi wa Simba kuona anaweza kuwa chaguo sahihi la muda la kuongoza timu hiyo yenye historia kubwa barani Afrika katika kipindi hiki kigumu ambacho inapitia huku ikikabiliwa na michezo muhimu miwili.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Simba inataka kuhakikisha haina pengo kubwa la kiufundi wakati huu ambao mashindano ya ndani na yale ya kimataifa yameanza kushika kasi. Wekundu wa Msimbazi wanatambua umuhimu wa kuendelea kuwa na mtu sahihi kwenye benchi la ufundi, ili kuendeleza falsafa ya ushindi na kuipa timu uthabiti katika mbio za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu na kufika mbali katika michuano ya CAF Champions League.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Endapo mpango huu utafanikiwa, Hemed Morocco atakuwa na jukumu la kusimamia kikosi hicho kwa muda mfupi huku akiweka msingi wa nidhamu na mbinu bora za kiufundi. Hatua hii pia inaweza kuwa sehemu ya kumpa uzoefu zaidi katika soka la klabu kubwa, huku akibaki na heshima kubwa kutokana na mafanikio yake katika ngazi ya timu ya taifa.
Mashabiki wa Simba wamepokea tetesi hizi kwa mitazamo tofauti. Baadhi wanaona ni nafasi nzuri ya kujaribu mbinu za kocha wa nyumbani, huku wengine wakisisitiza kuwa klabu inapaswa kumleta haraka kocha mwenye jina kubwa kimataifa. Hata hivyo, hadi sasa uongozi wa Simba haujatoa tamko rasmi, lakini dalili zote zinaonyesha kuwa Morocco anaweza kuwa chaguo la dharura la wekundu wa Msimbazi.
Kwa hali inavyoonekana, mjadala kuhusu nani atakayeongoza benchi la ufundi la Simba SC unazidi kushika kasi, na macho yote sasa yameelekezwa kwa mabosi wa Msimbazi na kocha Hemed Morocco.
Hata hivyo kocha huyo inatajwa atajiunga na Simba sc yeye pekee bila benchi lake la ufundi ambapo ataungana na baadhi ya makocha wachache waliosalia klabuni hapo akiwemo Selemani Matola na kocha wa viungo raia wa Afrika Kusini.