Home Soka Mwalimu Atua Simba Sc

Mwalimu Atua Simba Sc

by Dennis Msotwa
0 comments

Mashabiki wa klabu ya Simba Sc sasa mkae mkao wa kula baada ya mabosi wa klabu hiyo kupambana na kukamilisha usajili wa mshambuliaji hatari kutoka Tanzania, Selemani Mwalimu ambaye ametua kwa mkopo akitokea mabingwa wa Morocco, Wydad Athletic Club (WAC).

Habari hii imeleta msisimko mkubwa mitaani na mitandaoni, huku mashabiki wa Simba wakiamini ujio wa Mwalimu utakuwa silaha ya moto kwenye mbio za Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa ya CAF Champions League.

banner

Mwalimu, ambaye amewahi kuzichezea timu ya Singida Black Stars na Fountain Gate Fc za hapa nchini kisha kutua Wydad anatambulika kwa kasi yake ya kushambulia na uwezo wa kufumania nyavu ambapo amesaini dili la mkopo la msimu mzima wa 2025-2026 nafasi ya kuvaa jezi nyekundu kwa msimu huu.

Akizungumza baada ya kukamilisha usajili huo straika huyo alisema:

“Simba ni klabu kubwa, yenye historia na mashabiki wa aina yake. Nimekuja kuongeza nguvu na kuhakikisha tunafanikisha malengo ya kutwaa mataji makubwa. Najua presha ipo, lakini hii ndiyo nafasi yangu ya kuonyesha thamani yangu.”

Kwa upande wake, mmoja wa viongozi wa Simba SC amethibitisha kuwa Mwalimu atakuwa sehemu ya kikosi kitakachoanza maandalizi ya mechi ngumu zijazo wakianza na Ngao ya jamii dhidi ya Yanga sc kisha mechi za hatua ya awali ya Caf Champions League.

“Tulihitaji kuongeza makali ya ushambuliaji na Mwalimu ni jibu sahihi. Ni kijana mwenye njaa ya mafanikio, na tunajua ataendana na falsafa ya kocha wetu Fadlu Davis ambaye alisema anahitaji mshambuliaji mwenye sifa ya X-Factors,” alisema kiongozi huyo.

Kwa mashabiki wa Msimbazi, huu ni ujio wa “mwana nyumbani” anayetarajiwa kuongeza kasi ya mashambulizi sambamba na washambuliaji waliopo.

Tayari mitandao ya kijamii ya klabu ya Simba Sc imefurika jumbe za kumkaribisha baada ya kutambulishwa rasmi kupitia kurasa hizo na mashabiki wakiahidi kujitokeza kwa wingi kumshuhudia akianza kucheza chini ya jezi nyekundu.

Simba SC msimu huu  imejipanga kutwaa kila taji lililo mbele yao, sasa inaonekana kupeleka ujumbe kwa wapinzani wao wa jadi Yanga SC na wapinzani wa kimataifa kwamba safari ya Msimbazi msimu huu si ya masihara hasa baada ya kufanya sajili za maana kabisa.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited