Klabu ya Simba Sports Club imejikuta katika wakati mgumu baada ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kuiadhibu kwa jumla ya faini ya Dola 85,000 za Kimarekani, sawa na zaidi ya Shilingi milioni 220 za Kitanzania, kutokana na matukio mbalimbali yaliyotokea katika mechi za kimataifa zilizopita pamoja na kucheza bila mashabiki katika mchezo mmoja wa Caf.
Faini kubwa ya Dola 50,000 (zaidi ya TSh 120 milioni) ilitokana na tukio lililotokea katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry ya Misri, ambapo shabiki mmoja alivamia uwanja na kusababisha usumbufu, huku baadhi ya mashabiki wengine wakionekana kuwasha moto maeneo ya jukwaani—kitendo kilichochukuliwa kama tishio la kiusalama na uvunjifu wa nidhamu na CAF.
Aidha, katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya RS Berkane ya Morocco uliofanyika katika uwanja wa New Amaani Complex Visiwani Zanzibar, Simba ilitozwa faini nyingine ya Dola 35,000 kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni matukio ya vurugu na ukiukwaji wa taratibu za mchezo.
Kutokana na makosa hayo, Simba SC imetakiwa kulipa jumla ya Dola 85,000—kiasi kikubwa ambacho kimeleta changamoto kwa uongozi wa klabu hiyo kongwe nchini.
Mbaya zaidi, adhabu hiyo imeambatana na marufuku ya mashabiki kuhudhuria mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana, uliopangwa kuchezwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema klabu hiyo imesikitishwa na adhabu hizo, lakini imeamua kukabiliana nazo kwa njia chanya. Ametoa wito kwa mashabiki na wanachama wa Simba kuungana na klabu yao katika kipindi hiki kigumu kwa kuchangia sehemu ya faini hiyo.
““Nipo hapa kuwathibitishia kwamba mechi yetu ya Jumapili haitakuwa na mashabiki kutumikia adhabu ya CAF. Kilichosababisha ni mchezo ni dhidi ya Al Masry, kuna shabiki aliingia uwanjani na kuna mashabiki waliwasha moto. Adhabu hiyo inakwenda pamoja na faini ya Dola 50,000 kama Tsh. 120 milioni hivi.” alisema Ahmed Ally.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
“Wapo mashabiki ambao wametaka kuwa sehemu ya maumivu ambayo tunapitia Klabu ya Simba na maumivu yenyewe ni faini ya Tsh. 212,500,000 sawa na USD 85,000. Kwa mapenzi yao mashabiki wameomba kuchangia faini ili kuipunguzia klabu mzigo na sisi tumepokea na tumeridhia mashabiki wachangie hususani kwenye eneo la faini.”- Aliendelea kusema Semaji Ahmed Ally.
Pia, aliongeza kuwa michango ya mashabiki itasaidia kupunguza mzigo wa kifedha uliotokana na adhabu hizo, na kuisaidia klabu kuendelea kujiandaa kwa hatua zinazofuata za michuano ya kimataifa.
Hii si mara ya kwanza kwa Simba SC kukumbwa na adhabu za CAF kutokana na matukio ya mashabiki wake. Hali hiyo imeibua mjadala miongoni mwa wadau wa soka nchini, wakitaka kuwepo kwa elimu zaidi kwa mashabiki kuhusu umuhimu wa kufuata taratibu na nidhamu ya michezo, hasa katika mechi za kimataifa.
Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa kwenye mchezo wa Jumapili ambapo Simba itahitaji ushindi ili kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, licha ya kukosa uungwaji mkono wa mashabiki wake uwanjani.
Kwa upande wa mashabiki, wengi wameonesha moyo wa kujitolea na wameanza kuhamasishana mitandaoni kuchangia faini hiyo. Kampeni mbalimbali zimeanzishwa kwa nia ya kuiokoa klabu yao pendwa isitikisike kifedha.
Simba SC, licha ya changamoto hizi, inaendelea kuonesha kuwa ni klabu yenye misingi imara ya umoja, mshikamano na mapenzi ya dhati kutoka kwa mashabiki wake. Wakati CAF ikiweka msimamo wake kwa mujibu wa kanuni, Simba nayo inaweka historia ya kuonesha namna jamii ya wapenzi wa soka inavyoweza kushirikiana katika nyakati ngumu.