Kikosi cha mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, kimeondoka rasmi leo asubuhi Oktoba 16, 2025, kuelekea Malawi kwa ajili ya mchezo wao wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji Silver Strikers. Safari hiyo imeanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, huku mashabiki wa timu hiyo wakitoa hamasa ya nguvu kwa wachezaji kabla ya kupanda ndege.
Mechi hiyo ya kwanza kati ya miamba hao wa Tanzania na Malawi inatarajiwa kupigwa Jumamosi ya Oktoba 18, 2025, kwenye Uwanja wa Bingu National Stadium, mjini Lilongwe. Ni mchezo wa hatua ya mtoano kuelekea hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, na tayari unatazamwa kama kipimo cha nguvu na uzoefu kwa Yanga SC kwenye mashindano ya kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya safari hiyo, Ofisa Habari wa Yanga SC, Ali Kamwe, amesema kuwa ingawa timu ina matumaini makubwa ya kufanya vizuri, haitegemei mteremko wowote nchini Malawi, hasa ikizingatiwa kuwa kocha msaidizi wa Yanga, Patrick Mabedi, anatoka nchini humo na amewahi kuwa kocha wa timu ya taifa ya Malawi.
“Ni kweli tuna kocha msaidizi Patrick Mabedi ambaye anatoka Malawi, lakini hiyo haitufanyi tuone kama mechi hii itakuwa rahisi. Wachezaji wa Silver Strikers watajitahidi sana kuonyesha uwezo wao mbele ya kocha huyo ambaye ni mtu maarufu nchini kwao. Wanajua Mabedi anatujua vizuri, lakini pia wao wanataka kumuonyesha kuwa wamekua na kubadilika,” alisema Kamwe kwa kujiamini.
Hata hivyo, Kamwe hakusita kuonyesha imani yake kwa kikosi cha Yanga SC, akisisitiza kuwa timu hiyo imejiandaa kwa hali na mali kuhakikisha inaondoka Malawi ikiwa na matokeo chanya kabla ya mchezo wa marudiano utakaochezwa jijini Dar es Salaam wiki mbili zijazo.
“Tuna kikosi kipana, wachezaji wetu wako fiti na morali iko juu. Tumejiandaa vizuri na benchi la ufundi lina mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunapata ushindi au angalau matokeo mazuri ya ugenini. Mashabiki wetu wasiwe na shaka, Yanga ni timu kubwa na tuna malengo makubwa msimu huu,” aliongeza Kamwe.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Katika msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika, klabu hiyo iliishia hatua ya makundi jambo ambalo limewapa wachezaji na benchi la ufundi ari mpya ya kuendeleza mafanikio hayo. Safari yao ya mwaka huu imejaa matumaini ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa na kuandika historia nyingine barani Afrika.
Taarifa kutoka kambini zinaeleza kuwa kocha mkuu Roman Folz amefurahishwa na hali ya kiafya ya wachezaji wake ikiwemo kurejea kwa Clement Mzize pamoja na kiwango cha mazoezi, na huenda akaanza na kikosi chake cha kawaida kilichompa mafanikio kwenye hatua ya awali ya mashindano haya.
Mashabiki wa Yanga kutoka Tanzania na walioko Malawi wameonyesha dalili za kujitokeza kwa wingi siku ya mechi, kuhakikisha wanatoa sapoti kwa timu yao ya taifa isiyo rasmi. Kwa sasa, macho na masikio ya wanayanga yameelekezwa Lilongwe, ambako matumaini ya ushindi yanaonekana kuongezeka kadri siku ya mchezo inavyokaribia.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, Yanga inatarajiwa kufanya mazoezi rasmi ya mwisho kwenye Uwanja wa Bingu Ijumaa jioni, muda mfupi baada ya kuwasili. Mazoezi hayo yatatumika pia kama sehemu ya maandalizi ya mwisho ya kiufundi na kumalizia mbinu za kukabiliana na wapinzani wao.
Kwa sasa, ni jambo la kusubiri kuona kama vijana wa Folz wataweza kuendeleza moto wa mafanikio yao Afrika au kama Silver Strikers watawashtua Wana Jangwani mbele ya mashabiki wao wa nyumbani. Kitu kimoja ni wazi: mechi hii haitakosa ushindani, presha, na burudani ya kiwango cha juu.