Katika miaka ya hivi karibuni, soka la Tanzania limekuwa kivutio kikubwa kwa makocha kutoka mataifa mbalimbali ya Ulaya, Amerika Kusini na hata Afrika ya Kaskazini.
Klabu kubwa kama Simba SC na Yanga SC zimekuwa mstari wa mbele kuwaleta makocha wenye mbinu za kisasa na uwezo mkubwa wa kusimamia vipaji vya wachezaji. Hata hivyo, changamoto kubwa imekuwa pale makocha hao wanapopata nafasi kubwa zaidi baada ya muda mfupi tu nchini.
Tukumbuke mifano ya Sven Vandenbroeck aliyewahi kuinoa Simba SC, Sead Ramović aliyepita Yanga SC na kujiunga na CR Belouizdad ya Algeria, na sasa Fadlu Davis aliyeondoka Simba SC baada ya kupata ofa yenye maslahi makubwa kifedha na heshima zaidi kutoka Kaskazini mwa Afrika.
Sababu za Makocha Kuondoka
Kwanza kabisa, soka la Tanzania bado linatazamwa kama “daraja” la makocha kujiongezea CV na kuonekana kwenye ramani ya soka la Afrika ambapo Mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho yamekuwa jukwaa la kimataifa linalowapa nafasi ya kuonyesha uwezo wao. Mara tu wanapofanya vizuri dhidi ya vilabu vikubwa kutoka Kaskazini, jina lao linapanda thamani na wanapata ofa nono kutoka nchi zenye ligi tajiri zaidi.
Sababu ya pili ni masuala ya kifedha. Ligi za Algeria, Morocco, Tunisia na hata Misri zina bajeti kubwa zaidi ukilinganisha na klabu za Tanzania. Hivyo, ni vigumu kwa kocha kuendelea kusalia hapa endapo anapewa dau mara mbili au tatu ya mshahara wake wa awali.
Tatu, changamoto za kiutawala na miundombinu pia zinachangia. Wakati makocha wanapokuja Tanzania, mara nyingi wanakutana na changamoto za kiutendaji kama ucheleweshaji wa mishahara ya wachezaji, ukosefu wa vifaa vya kisasa vya mazoezi au kuingiliwa kwa majukumu yao na viongozi wa klabu. Hali kama hizi zinawafanya washawishike zaidi kukimbilia sehemu zenye mfumo bora zaidi.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Tanzania Ifanye Nini?
Kwanza, klabu zetu zinatakiwa kuwekeza katika sera za muda mrefu za makocha. Badala ya kusaini mikataba ya muda mfupi, kuwe na mikataba inayolinda maslahi ya klabu na kocha. Hii itasaidia kupunguza uwezekano wa makocha kuondoka ghafla.
Pili, lazima tuimarishe thamani ya ligi yetu. Hii ni pamoja na kuboresha miundombinu ya mazoezi, kuongeza udhamini, na kuhakikisha mishahara na stahiki za wachezaji na makocha zinalipwa kwa wakati.
Tatu, ni muhimu kujenga makocha wazawa. Tukizalisha makocha wenye uwezo wa kiwango cha juu ndani ya nchi, utegemezi wa makocha wa nje utapungua. Hii itafanya tunapopoteza kocha mgeni, bado ligi na timu zetu ziendelee kuwa imara.
Mwisho, serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinapaswa kushirikiana na klabu kubwa kuhakikisha tunaboresha hadhi ya ligi. Kadiri hadhi inavyopanda, ndivyo pia tutakavyoweza kuhimili mashindano ya kifedha na ligi za Kaskazini.
Kwa ujumla, tatizo la makocha kuondoka Tanzania si la kushangaza, kwani linaonyesha jinsi soka letu linavyokua na kuvutia macho ya dunia. Hata hivyo, kama taifa, tunapaswa kuweka mikakati thabiti kuhakikisha ukuaji huu unawanufaisha zaidi Watanzania na si tu wageni wanaopita.