Home Soka Yanga SC Yaanza Vyema Ligi Kuu NBC Kwa Ushindi wa Mabao 3-0 Dhidi ya Pamba Jiji FC

Yanga SC Yaanza Vyema Ligi Kuu NBC Kwa Ushindi wa Mabao 3-0 Dhidi ya Pamba Jiji FC

by Dennis Msotwa
0 comments

Klabu ya Young Africans SC (Yanga SC) imeanza kampeni zake za Ligi Kuu NBC Tanzania Bara msimu wa 2025/26 kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji FC katika mchezo uliopigwa leo kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Hata hivyo, licha ya ushindi huo, mashabiki wa Yanga walionekana kutoridhishwa na namna timu yao ilivyocheza kipindi cha kwanza kabla ya kocha Roman Folz kufanya mabadiliko yaliyobadilisha kabisa mchezo kwa kuwaingiza Pacome Zouzoua na Mohammed Doumbia.

Dakika za mwanzo za mchezo zilishuhudia Yanga SC ikikosa kasi na maelewano uwanjani. Kocha wa timu hiyo aliamua kuanza na Moussa Balla Conte na Lassine Kouma katikati ya uwanja, huku safu ya ushambuliaji ikiongozwa na Edmund John na Andy Boyeli. Licha ya wachezaji hawa kujaribu kushambulia, walionekana kukosa muunganiko mzuri, hali iliyosababisha mashabiki kuanza kuonyesha dalili za kutoridhika kupitia kelele na miluzi ya kuashiria presha kutoka majukwaani.

banner

Pamba Jiji FC walitumia udhaifu huo vizuri kwa kujaribu kucheza kwa nidhamu ya juu na kushambulia kwa kushtukiza, japokuwa hawakuweza kufunga kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Yanga iliyokua chini ya nahodha Bakari Mwamnyeto . Dakika zikiwa zinasogea, presha ya mashabiki ilionekana kuongezeka, wakitaka timu yao ianze kuonyesha ubora wanaoutarajia kutoka kwa mabingwa watetezi wa ligi hiyo.

Hata hivyo, mwishoni mwa kipindi cha kwanza, Yanga walipata mwanga. Katika dakika ya 45+4, Lassine Kouma aliwafurahisha mashabiki baada ya kufunga kwa kichwa akimalizia kona nzuri iliyochongwa kutoka wingi ya kushoto. Bao hilo lilileta tabasamu kwa mashabiki waliokuwa na wasiwasi, na Yanga ikaenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Yanga SC Yaanza Vyema Ligi Kuu NBC Kwa Ushindi wa Mabao 3-0 Dhidi ya Pamba Jiji-Sportsleo.co.tz

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi mpya baada ya kocha kufanya mabadiliko muhimu kwa kuingiza Mohammed Doumbia na Pacome Zouzoua, wachezaji ambao walionekana kuleta uhai kwenye safu ya kiungo na mashambulizi. Uhai huo ulidhihirika dakika ya 63 wakati Maxi Nzengeli alipoongeza bao la pili baada ya kumalizia krosi safi kutoka kwa beki Mohammed Hussein “Tshabalala”. Bao hili liliongeza presha kwa Pamba Jiji na kuwafanya mashabiki wa Yanga kupumua kwa furaha.

Mchezo uliendelea kwa Yanga SC kutawala dimba na kuonyesha ubora wa pasi na kasi katika mashambulizi. Juhudi zao ziliendelea kufika langoni mwa wapinzani na hatimaye dakika ya 90+2, Mudathir Yahaya aliihakikishia Yanga ushindi wa pointi tatu baada ya kufunga bao la tatu, akimalizia krosi nzuri ya Pacome Zouzoua ambaye alionekana kuibadili timu kwa kiwango chake cha juu.

Mashabiki walionekana kuridhika na sura mpya ya Yanga baada ya mabadiliko hayo, wakipongeza uwezo wa kiufundi wa wachezaji waliotoka benchi na kuboresha kiwango cha timu. Ushindi huu umeifanya Yanga SC kuanza msimu kwa kishindo huku ikishika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi kwa kuwa na pointi tatu na mabao matatu ya kufunga bila kuruhusu goli.

Kwa ushindi huu, Yanga SC imetuma ujumbe mzito kwa wapinzani wake kwamba bado ni timu ya kuogopwa msimu huu. Mashabiki sasa wanatarajia kuona kiwango bora zaidi katika mechi zinazofuata, hasa wakizingatia wingi wa wachezaji wapya waliopo kikosini na malengo makubwa ya kutetea taji la ligi na kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited