Home Soka Hersi Ateuliwa Ujumbe Fifa

Hersi Ateuliwa Ujumbe Fifa

by Dennis Msotwa
0 comments

Rais wa Klabu ya Yanga SC, Mhandisi Hersi Said amefungua ukurasa mpya wa historia kwa kuteuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano Yote ya Vilabu vya Wanaume Duniani kwa kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2025 hadi 2029.

Taarifa hiyo imethibitishwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ali Kamwe, ambaye amesema uteuzi huo ni heshima kubwa si tu kwa klabu ya Yanga, bali kwa taifa zima la Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Eng. Hersi anakuwa kiongozi wa kwanza kutoka eneo hilo kuingia katika kamati hiyo kubwa ya FIFA inayosimamia mashindano makubwa ya vilabu duniani.

Kamati hii ya FIFA ni miongoni mwa vyombo muhimu vinavyoratibu mashindano ya ngazi ya vilabu kama FIFA Club World Cup na mashindano mengine ya kimataifa, ikijumuisha ushiriki wa vilabu kutoka mabara yote. Kupitia nafasi hii, Hersi atakuwa na ushawishi katika kupanga na kusimamia kalenda ya mashindano, sheria na miongozo ya kiutendaji ya mashindano hayo.

Uteuzi wa Eng. Hersi unakuja wakati ambao amekuwa akihusishwa na mafanikio makubwa ndani ya klabu ya Yanga, ikiwa ni pamoja na kuifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho CAF mwaka 2023, pamoja na kuendelea kuitawala Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Uongozi wake umeleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji, kibiashara na kisoka ndani ya klabu hiyo kongwe nchini.

Kwa upande mwingine, uteuzi huu ni kielelezo cha namna viongozi wa soka Tanzania wanavyoanza kutambulika kimataifa kutokana na kazi kubwa wanayofanya ndani ya nchi. Wadau wa soka nchini wamempongeza Eng. Hersi kwa mafanikio hayo na kuona ni hatua ya kihistoria kwa soka la Tanzania kuwakilishwa katika ngazi ya juu kabisa ya uongozi wa mpira wa miguu duniani.

Kupitia ujumbe mfupi alioutoa, Hersi ameishukuru FIFA kwa imani waliyoionesha kwake na ameahidi kutumia nafasi hiyo kuwakilisha vyema Afrika Mashariki na Kati, pamoja na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya vilabu vya Afrika katika mashindano ya kimataifa.

Hivi karibuni pia Hersi aliteuliwa kuwa Rais wa chama cha vilabu barani Afrika (ACA) akiwa ni Rais wa kwanza wa chama hicho kilichoanzishwa kwa ajili ya kutetea maslahi ya vilabu barani Afrika hali iliyomfanya kuzidi kujiimarisha na kujisogeza kwa viongozi wakubwa wa soka duniani.

Kwa mafanikio haya, Eng. Hersi Said anazidi kuwa mfano wa kuigwa kwa viongozi vijana barani Afrika, na Tanzania inajivunia kuona kijana wake akishiriki moja kwa moja katika maamuzi makubwa ya mustakabali wa soka la vilabu duniani.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited