Mshambuliaji chipukizi wa Yanga SC, Clement Mzize, ameandika ukurasa mpya katika safari yake ya soka baada ya kuongeza mkataba wa mwaka mmoja, licha ya kupata ofa ya kuvutia kutoka kwa miamba wa Tunisia, Espérance Sportive de Tunis (ES Tunis).
Taarifa za ndani kutoka makao makuu ya Yanga, Jangwani, zinasema uongozi wa klabu hiyo umefanikiwa kumbakisha kinda huyo kwa juhudi kubwa, baada ya ES Tunis kuweka mezani dau nono lililokuwa tayari kumpa mchezaji maisha mapya barani Afrika Kaskazini.
Mzize, ambaye msimu uliopita alionyesha kiwango cha kuvutia kwa ukomavu na umakini katika safu ya ushambuliaji ya Wananchi akifunga mabao 13 katika ligi kuu ya soka ya Nbc, alikubali kuendelea na Yanga sc kwa kile alichokiita “kuendeleza ndoto zake akiwa nyumbani kabla ya kusaka changamoto kubwa zaidi barani na duniani.”
Sababu za Kutoondoka
Vyanzo vya karibu na mchezaji huyo vinadai kuwa uongozi wa Yanga ulimpa masharti bora ya kimaslahi ambapo atakua mchezaji mzawa anayelipwa zaidi nchini katika klabu hiyo na akiwa wa pili kwa nchi nyuma ya Feisal Salum na ahadi ya nafasi kubwa zaidi ya kucheza msimu huu, huku pia wakimshawishi kwa malengo ya timu katika mashindano ya kimataifa, hususani ligi ya Mabingwa Afrika.
Zaidi ya hapo, familia ya Mzize ilishauri kijana wao kusalia Jangwani kwa sasa, wakiamini bado ana nafasi ya kujifunza na kukua zaidi ndani ya mfumo wa Yanga ambao umempa heshima kubwa.
Umuhimu kwa Yanga
Mzize, licha ya umri mdogo, amekuwa silaha muhimu kwa kocha Miguel Gamondi kipindi akiifundisha timu hiyo na mpaka wakaja Sead Ramovic,Miloud Hamdi, akiwapa Wananchi aina ya mshambuliaji mwenye kasi, nguvu na uwezo wa kutumia nafasi chache alizopata.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Kocha Roman Folz pamoja na viongozi wa klabu hiyo wameungana na mashabiki wa Yanga sc kufurahia taarifa za mkataba mpya, wakiamini uwepo wa Mzize utazidi kuimarisha safu ya ushambuliaji pamoja na nyota wengine wakubwa wa kikosi hicho.
Neno la Makocha Waliowahi kumfundisha
Kocha Gamondi aliwahi kunukuliwa akisema “Mzize ni kijana mwenye kipaji cha kipekee. Ana njaa ya mafanikio na nidhamu kubwa mazoezini”.
Pia msemaji wa klabu hiyo Ally Kamwe alisema kuwa “Kumweka ndani ya kikosi chetu kwa msimu mwingine ni faida kwa Yanga na pia ni ishara kuwa tunajenga kikosi cha muda mrefu chenye wachezaji wazawa wenye uwezo mkubwa.”
Sa Itakuaje Hapo Jangwani Msimu Huu?
Kwa kusalia Yanga, Mzize sasa ataendelea kuishi ndoto za maelfu ya mashabiki wa klabu hiyo, huku akitarajiwa kuwa miongoni mwa nyota watakaobeba jukumu la kuipigania timu katika safari ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC na kufanya vizuri kimataifa akiungana na usajili mpya wa Celestine Ecua,Andy Boyeli,Offen Chikola katika eneo la ushambuliaji.
Kuwakataa ES Tunis ni uamuzi unaoweza kuonekana wa kishujaa kwa kijana mwenye ndoto kubwa, lakini pia ni ishara kwamba Yanga imebadilika – si klabu ya kuuza nyota mapema, bali ni taasisi inayojua namna ya kuwalinda na kuwajenga wachezaji wake.