Benki ya Crdb nchini ambao ndio wadhamini wakuu wa kombe la shirikisho nchini wamekana kudaiwa fedha za aina yeyote zinazohusu michuano hiyo kwa maana wao wameshalipa kwa mujibu wa utaratibu kupitia shirikisho la soka nchini (TFF).
Katika taarifa yao kwa umma iliyotolewa mapema leo baada ya jana Afisa habari wa Yanga sc kunukuliwa akisema kuwa kama hawajalipwa fedha hizo basi hawachezi fainali za michuano hiyo zitakazofanyika katika uwanja wa Amaani Visiwani Zanzibar Juni 28 mwaka huu.
“Benki ya CRDB inapenda kutoa ufanunuzi wa madai yaliyotolewa na msemaji wawklabu ya Yanga sc katika mkutano wake na wanahabari uliofanyika tarehe 09 Juni 2025 katika makao makuu ya klabu hiyo. Katika mkutano huo, msemaji wa klabu hiyo alinukuliwa akitoa taarifa kwa shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) na kwetu kama mdhamini mkuu wa mashindano ya kombe la shirikisho la benki ya CRDB kuwa Klabu ya Yanga haitocheza fainali za mashindano hayo msimu huu kama hawatolipwa fedha za ubingwa wa msimu uliopita”,Ilisomeka taarifa kutoka benki hiyo
“Tungependa kuufahamisha umma na wadau wote wa soka kuwa benki ya CRDB ni taasisi yenye kuzingatia weledi, kanuni na taratibu na kwa msingi huo tayari Benki ilikwisha tekeleza kikamilifu wajibu wake wa kifedha kwa TFF kama sehemu ya makubaliano ya udhamini wa mashindano haya hivyo malipo yote ya msimu uliopita yalifanyika kwa TFF kwa mujibu wa mkataba baina ya Benki ya CRDB na TFF”,Iliendelea kutiririka taarifa hiyo.
Kutokana na hilo hapa sasa shida imebaki kwa Shirikisho la soka nchini (TFF) kutoa taarifa kuhusu madai hayo ya klabu ya Yanga sc kutolipwa fedha hizo ambapo wameendelea na msimamo wao wa kutocheza mechi hiyo mpaka walipwe fedha hizo.