Mshambuliaji Kennedy Musonda amewaaga rasmi wanachama,wapenzi na Mashabiki wa klabu ya Yanga sc baada ya kumaliza mkataba wake na klabu hiyo huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya kwa pande zote.
Musonda ameitumikia Yanga sc kwa miaka mitatu akijiunga mwaka 2021-2022 wakati wa dirisha dogo akitokea klabu ya Power Dynamos ya nchini kwao Zambia.
“Wananchi niseme nini mmekua wa kipekee kwangu,familia yangu na kwa ndoto zangu,Asanteni kwa kucheka nami,kuota nami,kushinda nami na hata kulia nami”.
“Mtu mmoja alisema kila hadithi nzuri lazima ifike mwisho,nitawashukuru daima sasa ni wakati wa kuanza ukurasa mpya”,Ulisomeka ujumbe wa kuaga wa mshambuliaji huyo kupitia mtandao wake wa Instagram.
Yanga sc ilimnasa Mshambuliaji huyo ikiwapiku Tp Mazembe ambao nao walikua wanammendea kumsajili lakini fedha za GSM zilifanya dili hilo kukamilika kwa wakati na kuwapiga bao Mazembe.
Tangu awasili Yanga sc Musonda hajawahi kuwa mshambuliaji kiongozi katika klabu hiyo akifunikwa na kivuli cha Fiston Mayele na msimu huu amekua chini ya Prince Dube ambapo mara nyingi amekua akiingia kitokea benchi.