Klabu ya Simba umesisitiza kuwa mchezo namba 184 kati yao na Yanga Sc upo kama kawaida Juni 15, 2025 hivyo mashabiki wa klabu hiyo wajitokeze kwa wingi kuujaza uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mchezo huo umeingia katika mzozo baada ya Yanga sc kuendelea kusisitiza kuwa haitocheza mchezo huo mpaka pale matakwa yao yatakaposikilizwa ambapo pia watacheza kama mchezo huo utapangiwa tarehe nyingine.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa na uongozi wa klabu hiyo umesema kuwa mashabiki wajiandae kuingia uwanjani kwa tiketi zile zile walizokata machu 8 huku pia wale ambao hawajakata wasubiri utaratibu kutoka bodi ya ligi namna tiketi zitakavyopatikana.
“Tunawasihi msihadaike na kelele za mitaani,wale ambao walinunua tiketi za mechi ya tarehe 8/3/25 wazitunze kwa ajili ya mchezo huo na wale ambao hawajanunua tiketi wajiandae kununua baada ya tangazo la bodi ya ligi”,Ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo kutoka Simba Sc.
Hata hivyo taarifa hiyo imeonyesha kuungana na msimamo wa klabu ya Yanga sc ya kudai ripoti ya uchunguzi kuonyesha sababu kuu ya kutofanyika mchezo wa machi 8 2025.
“Tunaiomba bodi ya ligi na TFF watoe hadharani ripoti ya uchunguzi juu ya wale wote waliohusika kuharibu mechi ya Ligi jioni ya tarehe 7/3/2025 na Wachukuliwe hatua stahiki na mamlaka husika”.
“Kutotolewa kwa ripoti na kutokuchukuliwa hatua kwa wahusika wanaoendelea kunachochea ghasia ni sawa na kulinda uharamia katika mpira ambao unatia dosari mafanikio yaliyopo katika tasnia ya mpira wa miguu nchini”,Ilimalizikia kusomeka taarifa hiyo.
Mpaka sasa timu hizo mbili zinakinzana ambapo Yanga sc hawapo tayari kucheza huku Simba sc nao wakiwa tayari kushiriki mchezo huo.