Timu ya soka ya Yanga sc imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Nbc nchini baada ya kuifunga timu ya Namungo Fc kwa mabao 3-0 katika mchezo wa ligi kuu ya Nbc nchini uliofanyika katika uwanja wa Kmc Complex uliopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
Yanga sc imepata alama hizo tatu muhimu kupitia mabao ya Stephan Aziz Ki dakika ya 27 aliyefunga bao kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Namungo Fc Jonathan Nahimana baada ya kupokea pasi safi ya Maxi Nzengeli.
Prince Dube alifunga bao la pili kwa Yanga sc na la 13 kwake baada ya kumalizia pasi safi ya Kibwana Shomari aliyeambaa na mpira akiwazidi maarifa mabeki wa Namungo Fc ambapo mabao hayo mawili yalidumu mpaka kipindi cha mapumziko.
Kipindi cha pili Yanga sc waliendelea na msako wakilisakama lango la Namungo Fc ambapo dakika ya 74 Maxi Nzengeli alifunga bao la tatu akimalizia krosi ya Israel Mwenda.
Dakika 90 za mwamuzi Julias Mrope zilimalizika kwa Yanga Sc kuchukua alama tatu na kufikisha alama 73 wakijiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya Nbc wakicheza michezo 27 mpaka sasa.