Klabu ya Yanga Sc imethibitisha leo kushiriki kikao maalumu na bodi ya ligi kuu Tanzania kwa ajili ya kujadili masuala yahusuyo mchezo namba 184 wa ligi kuu ya Nbc dhidi ya Simba kilichofanyika katika ofisi za bodi ya ligi jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya leo Juni 9, 2025 iliyotolewa na kamati ya utendaji ya klabu hiyo imeeleza kuwa uongozi wa klabu hiyo umeshiriki kikao hicho kilichofanyika leo kwenye ofisi za bodi ya ligi Tanzania zilizopo jengo la NSSF mafao house, Dar Es Salaam, kuanzia saa 4:00 asubuhi na kubainisha kuwa imewasilisha msimamo wake kuwa haitashiriki mchezo huo mpaka pale matakwa yao yatakapotimizwa.
Kamati tendaji ya klabu hiyo inahitaji mambo manne yatekelezwe kabla ya timu hiyo kushiriki mchezo ambapo wanawataka Mtendaji Mkuu wa bodi ya ligi kujiuru pamoja na Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka nchini huku ikiwataka bodi iwe huru pamoja na takwa la mwisho ikitaka Kamati ya masaa 72 ivunjwe kutokana na kutokua na ufanisi.
Yanga sc wametoa taarifa kwa umma baada ya kutoka katika kikao hicho.
“Baada ya majadiliano ya saa kadhaa, Viongozi wa klabu waliwasilisha msimamo wa klabu yetu kuwa hatutashiriki mchezo namba 184 uliopangwa kufanyika tarehe 15 Juni 2025 mpaka pale matakwa yetu tuliyoyawasilisha kwa maandishi kwao yatakapotimizwa”,imesema sehemu ya taarifa hiyo.
“Tunawatakia kila la heri bodi ya ligi na shirikisho la mpira wa miguu nchini katika kushughulikia matakwa yetu yenye mustakabali mkubwa kwenye maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania”,ilisema sehemu ya taarifa hiyo
Mpaka sasa msimamo wa bodi ya ligi ni kwamba mchezo huo upo pale pale kama ulivyopangwa mpaka pale taarifa nyingine itakapotolewa.