Mashindano ya pikipiki ya Samia Motocross Championship yanatarajiwa kurejea kwa msimu wa pili kuanzia Julai 12, 2025, katika viwanja vya Lakilaki, Kisongo, Mkoani Arusha baada ya kumalizika kwa Msimu wa kwanza wa mashindano hayo yaliyofanyika mwezi Julai mwaka 2024.
Akizungumza leo 27 Mei, 2025 katika hafla ya kutangaza rasmi kuanza kwa msimu huo mpya, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, amesema mashindano haya si tu burudani bali ni kichocheo kikubwa cha uchumi kwa wakazi wa Arusha na yanatoa nafasi kwa vijana kujipatia kipato kupitia vipaji vyao vya kuendesha pikipiki, huku wakibadili mtazamo hasi uliokuwepo awali dhidi ya waendesha bodaboda.
“Mashindano haya yanasaidia kuinua heshima ya vijana waliokuwa wakionekana kama wahuni, kumbe ni watu wenye vipaji na malengo ya kujikimu kimaisha”. Amesema Mhe. Makonda.
Ameongeza kuwa, suala la usalama kwa washiriki litapewa kipaumbele, ambapo vifaa vyote muhimu vya usalama vitapatikana na kuzingatia viwango vya kimataifa.
Mashindano hayo yatajumuisha waendesha bodaboda ambapo mshindi wa kwanza atapata kiasi cha fedha shilingi milioni 5 pamoja na wale wataalam wa mbio maalum (experts) ambapo mshindi wa kwanza atapata shilingi milioni 15 na yatahusisha wananchi pamoja na washiriki kutoka ndani na nje ya Tanzania.