Klabu ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro imepata nguvu mpya kwenye benchi la ufundi baada ya kuthibitisha kujiunga rasmi kwa Kocha Raia wa Kenya, Yusuf Chipo, ambaye sasa ndiye kocha mkuu wa kikosi hicho chenye maskani yake Manungu, Turiani.
Chipo, ambaye ana uzoefu wa kutosha katika soka la Afrika Mashariki, anachukua nafasi hiyo huku akisaidiwa na Kocha Awadh Juma maarufu kama Maniche, ambaye aliiongoza timu hiyo katika mechi mbili za mwanzo za Ligi Kuu ya NBC msimu huu. Katika mechi hizo, Mtibwa Sugar ilifanikiwa kushinda moja na kupoteza moja, matokeo yaliyotia moyo lakini pia yalionyesha hitaji la maboresho zaidi katika kikosi hicho.
Awali, Chipo alitarajiwa kujiunga na Mtibwa mwanzoni mwa msimu, lakini alikumbwa na matatizo ya kifamilia yaliyomzuia kuwasili kwa wakati. Sasa akiwa ameripoti rasmi Morogoro na tayari ameanza kazi, Kocha huyo anatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika kikosi hicho ambacho kimekuwa na msimu migumu katika miaka ya karibuni.
Chipo ni kocha mwenye falsafa ya soka la kasi, lenye nidhamu ya hali ya juu na akiamini sana katika vipaji vya wachezaji vijana. Katika safari yake ya ukufunzi, amewahi kuinoa klabu ya Mulanga Seals ya Kenya na pia Coastal Union ya Tanga, ambako alionyesha uwezo mkubwa wa kukuza vipaji na kuleta ushindani wa hali ya juu.
Kwa sasa, tayari ameanza mazoezi na kikosi cha Mtibwa Sugar, ambapo ameonekana kuwa na mawasiliano ya karibu na wachezaji, akiwataka kutoa asilimia 100 kila mara wanapovaa jezi ya timu hiyo. Vilevile, taarifa kutoka ndani ya timu zinaeleza kuwa kocha huyo ameanza kufanya tathmini ya wachezaji wake wote, kwa lengo la kujua ni nani anaweza kumsaidia kufikia malengo yake msimu huu.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Uongozi wa Mtibwa Sugar umeeleza matumaini makubwa kwa Kocha Chipo, wakiamini kuwa ataweza kuiweka timu katika mstari mzuri wa ushindani na kuwarejeshea mashabiki furaha waliyoikosa kwa muda mrefu. Aidha, ujio wake umepokelewa kwa shangwe na wapenzi wa soka Morogoro, hasa kwa kuzingatia historia yake ya kupendelea soka la kushambulia na kutumia vipaji chipukizi.
Katika mahojiano mafupi baada ya kuwasili kwake, Kocha Chipo alieleza kuwa anafurahia kujiunga na Mtibwa Sugar na anaamini timu hiyo ina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri. “Mtibwa ni klabu yenye historia na heshima kubwa nchini Tanzania. Najua haitakuwa kazi rahisi, lakini nina imani tutafanya makubwa,” alisema Chipo kwa kujiamini.
Kikosi cha Mtibwa Sugar kinatarajiwa kushuka dimbani wikiendi hii kuendelea na kampeni ya Ligi Kuu, ambapo mashabiki watakuwa na macho kwa Kocha Chipo kuona ni namna gani ataanza safari yake rasmi ya kuiongoza timu hiyo msimu huu.