Home Soka MFUMO UMEKUBALI: YANGA SC KUKAMILISHA KAZI DHIDI YA WILLIETE BENGUELA MKAPA

MFUMO UMEKUBALI: YANGA SC KUKAMILISHA KAZI DHIDI YA WILLIETE BENGUELA MKAPA

by Dennis Msotwa
0 comments

Klabu ya Yanga SC kesho Jumamosi inatarajia kushuka dimbani katika mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Williete Benguela FC ya Angola, mchezo utakaopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Ni mchezo muhimu kwa mabingwa hao wa Tanzania ambao wapo katika nafasi nzuri baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 wakiwa ugenini nchini Angola, hivyo kesho wanahitaji kutamalaki dakika 90 pekee ili kufanikisha safari yao kuelekea hatua ya pili ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika.

Uongozi wa Yanga SC umelipa mchezo huo ladha ya kipekee kwa kuupa kauli mbiu ya “MFUMO UMETIKI”, kauli inayolenga kuhamasisha mashabiki kujitokeza kwa wingi kuijaza Benjamin Mkapa na kushuhudia burudani kabambe ambayo viongozi wa klabu hiyo wameahidi. Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa Yanga SC Ally Kamwe alisema mchezo wa kesho si wa kawaida, kwani mashabiki watashuhudia mambo ya kipekee ambayo hayajawahi kufanyika.

banner

“Tumekuja na kauli mbiu ya MFUMO UMETIKI maalum kwa ajili ya mchezo wa kesho tu. Tuna jambo la tofauti mtaliona mkija Uwanja wa Mkapa. Kuna moto mkali sana utawashwa kesho. Uongozi umeweka viingilio vya kirafiki kabisa kuhakikisha kila shabiki anapata nafasi ya kuishangilia timu yake. Mzunguko ni Shilingi 3,000 tu, VIP C Shilingi 10,000, VIP B Shilingi 20,000 na VIP A Shilingi 30,000. Hii yote ni kwa ajili ya kuhakikisha tunakuja kwa wingi kuisapoti timu yetu,” alisema msemaji huyo.

Zaidi ya maandalizi ya mashabiki, upande wa benchi la ufundi pia umeweka wazi mkakati maalum kuelekea mchezo huo. Kocha mkuu wa Yanga SC, Roman Folz, amesema licha ya ushindi wa ugenini kuwaweka kwenye nafasi nzuri, bado wanauchukulia mchezo huu kwa uzito mkubwa. Folz amesisitiza kuwa atatumia wachezaji watakaokuwa tayari kwa mchezo, huku akieleza kuwa mpango wake wa “rotation” utaendelea kama kawaida ili kuhakikisha kila mchezaji anapata nafasi na timu inabaki na ushindani mkubwa.

“Tunajua tuna faida ya mabao matatu, lakini hilo halitufanyi kupunguza nguvu. Tunahitaji kushinda tena nyumbani na kuendelea kujenga morali ya wachezaji na mashabiki. Wachezaji wote walioko tayari watahusika, rotation ni muhimu katika timu yenye msimu mrefu na yenye malengo makubwa. Hivyo mashabiki wakae tayari kuona kikosi chenye hamasa na dhamira moja – kushinda na kufuzu,” alisema Folz.

Mashabiki wa Yanga SC wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi, wakisukumwa na kiu ya kuendelea kushuhudia mafanikio ya timu yao ambayo imekuwa ikiwapa burudani na heshima kubwa katika miaka ya karibuni. Kauli mbiu ya “MFUMO UMEKUBALI” imeshaongeza hamasa mitaani na mitandao ya kijamii, huku wapenzi wa soka wakiweka wazi matarajio yao ya kuona burudani kubwa kesho.

Kwa matokeo ya 3-0 ugenini, Yanga SC ipo katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya pili, lakini kesho ni fursa kwa timu hiyo kuonyesha ukubwa wake mbele ya mashabiki wake nyumbani na kuendeleza moto wa ushindani katika safari ya kutafuta heshima ya bara. Bila shaka, kesho Benjamin Mkapa utakuwa jukwaa la shamrashamra, burudani na furaha ya kijani na njano, kwani kwa Yanga SC mfumo umetiki, kazi imebaki kukamilisha tu.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited