Utata umezuka jangwani kuhusu wachezaji waliotolewa kwa mkopo na klabu hiyo wakati wa dirisha dogo kufuatia baadhi ya wachezaji kuigomea klabu hiyo kufuatia kutoshirikishwa katika kuchagua timu za kuhamia.
Wakati Ali Ali akifunguka na kugoma kuwasili katika timu ya Jkt Tanzania utata umetanda kuhusu Rafael Daud baada ya kutowasili katika klabu ya Singida United alipotolewa kwa mkopo huku kukiwa hakuna taarifa zozote kuhusu mahali alipo kiungo huyo.
Daud aliyejiunga na Yanga akitokea klabu ya Mbeya City bado hajawasili katika klabu ya Singida united licha kutosikika malalamiko yeyote kuhusu kutoka kwake.
Mkurugenzi wa Singida United Festo Sanga amethibitisha kutowasili kwa mchezaji huyo licha ya kukamilisha kila kitu kwa Yanga.
Akijibu kuhusu tuhuma hizo Hassan Bumbuli ambaye ni Afisa Habari wa klabu ya Yanga amesisitiza kuwa mchezaji ambaye hajaridhika na uamuzi huo anatakiwa aripoti makao makuu ya klabu hiyo kwa ufafanuzi zaidi.