Home Soka Simba Sc Yaingia Kinyan’ganyiro Cha Klabu Bora Afrika

Simba Sc Yaingia Kinyan’ganyiro Cha Klabu Bora Afrika

by Dennis Msotwa
0 comments

Ni rasmi sasa Simba Sports Club ya Tanzania imeandika ukurasa mwingine wa dhahabu katika historia yake baada ya kutajwa kwenye orodha ya klabu 10 bora barani Afrika zinazowania Tuzo ya Klabu Bora ya Mwaka 2025 inayotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na CAF, Simba SC imeingia katika orodha hiyo ya heshima kubwa sambamba na vigogo wa soka la Afrika akiwemo Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Pyramids FC (Misri), RS Berkane (Morocco), Asec Mimosas (Ivory Coast), Orlando Pirates (Afrika Kusini), Stellenbosch FC (Afrika Kusini), CS Constantine (Algeria), CR Belouizdad (Algeria) na Al Hilal SC (Sudan).

SIMBA YAENDELEA KUNG’ARA AFRIKA

Uteuzi huu wa Simba SC si wa bahati nasibu, bali ni matokeo ya kazi kubwa, nidhamu na ubora wa timu hiyo katika msimu uliopita, ambapo ilifanya kile ambacho vilabu vingi vya Afrika Mashariki vimeshindwa kwa muda mrefu  kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) msimu uliopita.

banner

Wawakilishi hao wa Tanzania walikuwa moto wa kuotea mbali msimu wa 2024/2025, wakitoa vilabu vikubwa barani Afrika katika safari yao ya kusaka ubingwa kabla ya kupoteza kwa mabao 2-0 kwa RS Berkane ya Morocco kwenye fainali iliyochezwa jijini Rabat na kutoa sare ya 1-1 katika fainali ya pili Visiwani Zanzibar.

Hata hivyo, licha ya kupoteza taji hilo, Simba ilionyesha ubora wa hali ya juu, ikionesha kandanda safi lililovutia wadau wengi wa soka barani Afrika. Ilikuwa ni timu yenye mpangilio, nidhamu, na ubunifu mkubwa jambo lililovutia macho ya CAF na kuifanya ichaguliwe kuwania heshima hii kubwa.

Simba Sc Yaingia Kinyan'ganyiro Cha Klabu Bora Afrika-www.sportsleo.co.tz

HESHIMA KWA UKANDA WA CECAFA

Kwa mujibu wa CAF, Simba ndiyo klabu pekee kutoka Ukanda wa CECAFA (Afrika Mashariki na Kati) kuingia kwenye orodha hiyo, jambo linaloipa Tanzania hadhi kubwa katika ramani ya soka la Afrika.

Ni ishara kwamba kazi kubwa inayofanywa na viongozi, benchi la ufundi na wachezaji wa Simba imeanza kuzaa matunda. Uwekezaji uliofanywa katika miundombinu, usajili wa kimataifa na utendaji wa kitaalamu unaifanya Simba kuwa klabu ya mfano barani.

“Hii ni heshima kubwa kwa Simba na kwa Tanzania nzima. Tulianza safari kwa ndoto, na sasa tumeifikisha nchi yetu kwenye ramani ya soka la dunia,” ilisema taarifa iliyochapishwa na mitandao ya kijamii ya klabu hiyo.

Simba Sc Yaingia Kinyan'ganyiro Cha Klabu Bora Afrika-www.sportsleo.co.tz

SAFARI YA KIHISTORIA

Simba ilianza kampeni zake za Kombe la Shirikisho msimu uliopita kwa kishindo kikubwa, ikiongozwa na wachezaji kama Joshua Mutale,Ellie Mpanzu na Shomari Kapombe ambaye pia ameingia kwenye orodha ya wachezaji bora wa mwaka Afrika (CAF Home-Based Player of the Year).

Timu hiyo ilishinda michezo mikubwa dhidi ya Misri,Al-Masry ya Misri, na Stelleboch Fc ya Afrika Kusini, kabla ya kupenya hadi fainali – rekodi ambayo haijawahi kuwekwa na timu yoyote ya Tanzania katika mashindano ya CAF.

Katika michezo hiyo, Simba ilionyesha umoja, nidhamu na uthabiti wa hali ya juu. Kocha mkuu, Fadlu Davies, alisifiwa kwa mbinu zake za kisasa na uchezaji wa kushambulia uliowafanya watani wao wa jadi, Yanga SC, kuanza kujipanga upya ili kuifikia Simba katika kiwango cha kimataifa.

Simba Sc Yaingia Kinyan'ganyiro Cha Klabu Bora Afrika-www.sportsleo.co.tz

CAF YAITAMBUA SIMBA

Kwa mujibu wa vyanzo vya ndani vya CAF, vigezo vilivyotumika katika uteuzi huu ni pamoja na mafanikio ya kimashindano, ubora wa kiufundi, usimamizi bora wa klabu, na mchango wake katika kukuza taswira ya soka la Afrika.

Simba imepata alama nyingi kutokana na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho, rekodi nzuri ya mashabiki, na miundombinu ya kisasa ikiwemo Uwanja wa Mo Simba Arena na kituo cha mafunzo ya vijana Simba Soccer Academy.

MASHABIKI WASHANGILIA

Habari hizi zimepokelewa kwa shangwe kubwa na mashabiki wa Simba, wakitumia mitandao ya kijamii kusherehekea mafanikio hayo. Hashtag kama #SimbaNiBoraAfrika na #PrideOfTanzania zimeanza kutrendi, wengi wakisema hii ni heshima kwa taifa zima.

MWISHO WAKE

Kwa sasa, macho yote yako kwenye sherehe za utoaji wa tuzo hizo za CAF zitakazofanyika baadaye mwaka huu, ambapo mashabiki wa Simba wanaamini klabu yao ina nafasi kubwa ya kushinda kutokana na msimu wake wa mafanikio makubwa.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited