Klabu ya Simba sc imefanikiwa kuingia makubaliano na kampuni ya bia ya Serengeti ya udhamini kupitia kinywaji cha Prisner Lager kwa muda wa miaka mitatu wenye thamani ya pesa za kitanzania shilingi bilioni moja na nusu.
Katika udhamini huo kampuni hiyo itatumia nembo na picha za wachezaji wa klabu hiyo katika matangazo yake ambapo itafaidika na kupanda kwa mauzo huku Simba sc itafaidika na fedha hizo katika uendeshaji wa klabu hiyo.
Katika hafla hiyo klabu ya Simba sc iliwakishwa na Afisa Mtendaji mkuu wa klabu hiyo Iman Kajula pamoja na wajumbe wa bodi ya klabu hiyo Asha Baraka na Raphael Chegeni.
“Hili ni tukio la kihistoria. Katika mechi zote ambazo Simba inacheza mtaani kunanona na naamini Pilsner Lager kuwa mshirika wa Simba hata mauzo yataongezeka. Mashabiki wa Simba wanapenda kujipa raha. Tunaamini ushirikiano huu utazidi kutujenga. Tunawaahidi kupitia Simba bia itakuwa maarufu zaidi.” Alisema mjumbe wa Bodi, Raphael Chegeni
Kwa upande wa kampuni ya bia ya Serengeti yenyewe mbali na Mkurugenzi wa Masoko Anitha Rwehumbiza,Pia iliwakilishwa na mkurugenzi mtendaji Obinna Anyalebechi ambaye alisema kuwa “Tunajivunia kuziunganisha taasisi mbili kubwa za SBL na Simba kwa mkataba wa udhamini wa miaka mitatu. Kupitia udhamini huu utaifanya bia yetu ya Pilsner Lager kuwa mdhamini wa Simba.”