Simba SC Yatinga Hatua ya Pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika Licha ya Sare Dhidi ya Gaborone Unite
Klabu ya Simba SC imefanikiwa kutinga hatua ya pili ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Gaborone United ya Botswana katika mchezo uliochezwa bila mashabiki kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Matokeo hayo yameifanya Simba SC kusonga mbele kwa jumla ya ushindi wa mabao 2-1, ikikumbukwa kuwa katika mchezo wa kwanza ugenini jijini Gaborone, Wekundu wa Msimbazi walishinda kwa bao 1-0.
Mchezo wa marudiano ulikuwa na presha kubwa kwa pande zote mbili, huku Simba ikihitaji angalau sare ili kufuzu, wakati Gaborone walihitaji ushindi ili kuendeleza safari yao ya michuano hiyo mikubwa barani. Dakika ya 45, Simba SC ilipata bao kupitia kwa Jean Charles Ahoua kwa mkwaju wa penalti. Penalti hiyo ilitokana na beki wa Gaborone United, Mourice Abraham, kumchezea rafu mshambuliaji wa Simba ndani ya eneo la hatari, na mwamuzi hakusita kuonesha nukta ya penati. Ahoua alikwamisha wavuni kwa utulivu mkubwa, na kupeleka Simba mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Gaborone United wakionekana kurejea kwa nguvu wakiwa na nia ya kusawazisha. Hatimaye dakika ya 58, walipata penalti baada ya beki wa Simba, Chamou Karabou, kumchezea rafu mshambuliaji wa wapinzani ndani ya eneo la hatari. Nahodha wa timu hiyo, Lebogang Ditsele, alifunga kwa ustadi na kuirejesha timu yake mchezoni. Bao hilo liliwapa moyo wachezaji wa Gaborone waliendelea kushambulia, lakini safu ya ulinzi ya Simba ilionekana kujipanga vyema zaidi hadi mwisho wa mchezo.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Licha ya kufuzu, mashabiki wa Simba SC bado wamekuwa na maswali kuhusu kiwango cha mchezo wa timu yao. Kocha wa muda, Hemed Morocco, amekuwa akiongoza kikosi hicho tangu kuondoka kwa Fadlu Davis, lakini bado hajafanikiwa kuipatia timu falsafa thabiti ya mchezo. Wadau wengi wa soka wanaona kuwa Simba inahitaji kuboresha safu yake ya ushambuliaji na kuongeza ubunifu katika eneo la kati ili kuendana na changamoto zitakazojitokeza hatua zinazofuata.
Kwa matokeo haya, Simba SC sasa itasubiri kupangwa na mpinzani mwingine kwenye hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Ni wazi kuwa matarajio ya mashabiki wa Msimbazi ni kuona timu yao ikirejea kwenye kiwango cha juu kinachoweza kuwapa nafasi ya kufika mbali zaidi kwenye michuano hii mikubwa ya vilabu barani. Licha ya changamoto, Simba SC bado imeonesha uthabiti na uzoefu wa kimataifa unaoiwezesha kusonga mbele.