Table of Contents
Mashabiki wa soka nchini wanayo sababu ya kutabasamu! Uongozi wa Klabu ya Yanga SC umetangaza kugawa burudani buree katika uwanja wa Benjamini Mkapa baada ya uamuzi wa kishujaa na wa kipekee kuelekea mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers ya Malawi ambapo kiingilio kimeondolewa!
Ndiyo, umesikia vizuri. Kwa mara ya kwanza katika historia ya hivi karibuni ya michuano mikubwa barani Afrika, mashabiki wa Yanga wataingia Uwanja wa Benjamin Mkapa bure kabisa kushuhudia timu yao ikipigania tiketi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Awali, viingilio vilikuwa vimetangazwa ambapo kiwango cha chini kilikuwa shilingi 5,000. Lakini baada ya kikao cha dharura kilichofanyika makao makuu ya klabu hiyo, uongozi wa Yanga chini ya Rais Hersi Said umeamua kufuta viingilio vyote isipokuwa VIP A na VIP B ambazo zimehifadhiwa kwa wageni maalum na wanachama wa “Black Card.”
Akizungumza kwa hisia kali mbele ya waandishi wa habari, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, alifunguka kuwa uamuzi huo haukuwa rahisi, lakini ulilazimishwa na mapenzi kwa mashabiki na umuhimu wa mchezo huo mkubwa.
“Tumekubaliana kuwa mechi hii imeondolewa viingilio majukwaa yote isipokuwa jukwaa la VIP A na VIP B ambayo yamehifadhiwa kwa waalikwa maalum na wanachama wetu wa Black Card,” alisema Kamwe.
“Ombi hili lilikuwa gumu sana kukubaliwa kwa sababu viongozi wetu wana majukumu makubwa ya kuiendesha timu, lakini tukatambua umuhimu wa mchezo huu – ushindi ndiyo kipaumbele chetu. Tunahitaji kila shabiki awe uwanjani kuisukuma timu yetu kushinda,” aliongeza kwa msisitizo.
WAZEE WA YANGA WAIPA TIMU SAPOTI NZITO
Habari zilizopatikana ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa uamuzi huu umetokana na ombi maalum la Wazee wa Yanga ambao mapema asubuhi ya Oktoba 21, 2025, walifika ofisini kwa uongozi na kuomba mechi hiyo iwe bure ili mashabiki wajitokeze kwa wingi.
Wazee hao waliweka wazi kuwa mechi hii ni ya maisha au kifo kwa kuwa Yanga ilipoteza mchezo wa kwanza nchini Malawi kwa bao 1-0, hivyo inahitaji sapoti ya kila Mwananchi kuibuka na ushindi utakaowaweka hatua ya makundi.
“Wazee walikuja na ombi la dhati kabisa, wakasema huu ni wakati wa umoja, sio biashara,” chanzo kimoja kutoka ndani ya Yanga kiliiambia Sportsleo. “Walisema kama kila shabiki atajitokeza, Mkapa itatikisa, na Silver Strikers hawatapata hata pumzi ya kupumua.”
MKAPA KUTIKISIKA KAMA ULIVYOZOELEKA
Tayari mitandao ya kijamii imejaa hamasa kubwa kutoka kwa mashabiki wa Yanga nchini kote ambapo mashabiki wa klabu hiyo kupitia matawi yao wameanza kampeni za kuchanga fedha za nauli kutoa mikoani kuja jijini Dar es salaam kuangalia mchezo huo, huku wapenzi wa soka wakiahidi kufurika uwanjani kwa maelfu.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Taarifa kutoka kamati ya maandalizi zinasema maandalizi ya usalama, ulinzi, na usafiri kwa mashabiki kutoka mikoa ya jirani yameanza kuimarishwa. Lengo ni kuhakikisha kila mtu anapata nafasi ya kuishangilia Yanga bila bughudha.
MASHABIKI WAHIMIZWA KUJITOKEZA KWA WINGI
Uongozi wa Yanga pia umetoa rai kwa mashabiki wote kuja kwa wingi wakiwa wamevaa jezi za njano na kijani, ili kugeuza Mkapa kuwa “bahari ya rangi ya Yanga.”
“Baada ya kusema hayo niwataarifu kuwa Mageti yatafunguliwa mapema kabisa kuanzia saa mbili asubuhi, naomba nisisitize hapa, Ombi hili limeombwa na Wanayanga na limepitishwa na Viongozi wa Yanga, kama wewe siyo Mwanayanga na ukaja na dhamira ya Hovyo basi niwaambie tu 𝐓𝐔𝐓𝐀𝐋𝐀𝐔𝐌𝐈𝐀𝐍𝐀, ni heri ukaja na ukatulia uangalie mpira, ukija na Ajenda tofauti basi tutaishi na wewe kwa Utofauti.
“Sisi kumbaini mtu asiyekuwa sehemu yetu ni rahisi sana, sisi tupo Vitani, tunakwenda kupambana kwaajili ya timu yetu, tunawaalika watu wote wanaopenda mpira, ukija na dhamira mbaya basi tutalaumiana nawaambia, kama huwezi kuja kwenye mechi yetu na ukatulia basi subiri timu yako ikicheza ukaangalie, sisi wenye timu yetu tuna kazi yetu ya Kufanya siku hiyo”Alisema Ally Kamwe mbele ya waandishi wa habari
YANGA INATAFUTA KUFUTA MACHOZI YA MALAWI
Mchezo huu wa marudiano unatarajiwa kuwa kivutio kikubwa kwa wapenzi wa soka. Yanga, chini ya kocha Patrick Mabedi, inaingia uwanjani ikihitaji ushindi wa angalau mabao mawili bila kuruhusu ili kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Baada ya matokeo ya 1-0 ugenini, mashabiki wa Yanga wanaamini uwanja wa Benjamini Mkapa utakua sehemu sahihi ya kufanya ”Comeback” ya uhakika ili kurejesha imani kwa mashabiki wake.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka benchi la ufundi, kikosi cha Yanga kipo kamili, nyota wote wakiwa fiti – akiwemo mshambuliaji hatari Clement Mzize aliyekua na majeraha, huku winga Maxi Mpia Nzengeli, na straika Prince Dube ambao wameahidi kupambana kufa na kupona kuhakikisha timu yao inafuzu.
MWISHO WAKE
Ni wazi kwamba Oktoba 25, 2025, Uwanja wa Benjamin Mkapa utageuka kuwa jukwaa la historia. Yanga imethibitisha kwa vitendo kuwa ni klabu ya watu “Timu ya Wananchi.” ambapo na kwa mashabiki, hii ni nafasi ya kipekee ya kuandika ukurasa mpya wa utukufu. Wote wanasubiri kuona kama uamuzi wa kuondoa viingilio utaleta matokeo makubwa zaidi kwa kufuzu hatua ya makundi ya klabu bingwa barani Afrika.