Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, wanatarajiwa kushuka dimbani kesho Jumatano, Oktoba 1, 2025, kuvaana na Namungo FC katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu. Mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 1 usiku, huku kila upande ukiwa na nia ya kuonyesha ubora na kutafuta pointi tatu muhimu.
Kwa Simba SC, huu utakuwa ni mchezo wao wa pili wa ligi baada ya kuanza msimu kwa ushindi dhidi ya Fountain Gate FC, huku wakiwa na kumbukumbu ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ambapo walifanikiwa kusonga mbele. Timu hiyo inarejea uwanjani ikiwa na morali ya juu, lakini wanatambua kuwa Namungo si timu ya kubeza.
Katika mkutano na waandishi wa habari leo, kocha msaidizi wa Simba SC, Seleman Matola, amekiri wazi kuwa mchezo huo hautakuwa mwepesi hata kidogo. “Wanatupaga game ngumu sana,” alisema Matola, akisisitiza kuwa Namungo inafundishwa na kocha Juma Mgunda ambaye anaelewa vyema falsafa ya Simba kutokana na historia yake na klabu hiyo. “Tunajua wanakuja kwa mbinu, na tumejiandaa kwa kila hali.”
Matola ameongeza kuwa licha ya kutengeneza nafasi nyingi kwenye mchezo uliopita, walishindwa kuzitumia vizuri kutokana na akili nyingi kuwa kwenye mechi ya kimataifa. Hata hivyo, amesema kikosi kipo tayari kwa mchezo wa kesho na dhamira yao ni kupata ushindi mbele ya mashabiki wao.
Kwa upande wake, mchezaji wa Simba, Anthony Mligo, ambaye aliwahi kuchezea Namungo, amesema anaufahamu vizuri mfumo wa timu hiyo na anajua wanavyopambana wanapokutana na vigogo. “Namungo ni timu inayobadilika kwenye mechi kubwa, lakini tumejiandaa vema na tupo tayari kwa vita,” alisema Mligo huku akisisitiza kuwa anataka kuonyesha thamani yake mbele ya timu yake ya zamani.
Namungo FC nao hawajabaki kimya. Kocha wao mkuu Juma Mgunda, ambaye ameiongoza timu hiyo kwenye michezo miwili ya ligi msimu huu, amesema maandalizi ya kukutana na Simba yamekamilika kwa asilimia 100. “Tunakwenda kucheza na timu nzuri yenye wachezaji bora, lakini tumejiandaa kwa changamoto hiyo. Tunajua tutakutana na mchezo mgumu, lakini hatubabaiki,” alisema Mgunda kwa kujiamini.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Mchezaji wa Namungo, Abdallah Mfuko, ameongeza kuwa wanaiheshimu Simba kama moja ya timu kubwa nchini, lakini wao wamekuja kwa ajili ya kupambana na kutafuta matokeo mazuri. “Tunajua ugumu wa mchezo, lakini tuna lengo la kuondoka na pointi, au angalau kuhakikisha tunatoa ushindani mkubwa,” alisema Mfuko.
Mchezo huu unatarajiwa kuwa wa kasi na burudani kubwa kutokana na historia ya ushindani kati ya timu hizi. Simba wanaingia na nguvu mpya baada ya kuimarika kwenye dirisha la usajili, huku Namungo wakitafuta ushindi wao wa pili msimu huu wakiwa tayari wamecheza michezo miwili.
Mashabiki wa soka nchini wanatazamia mchezo wa kusisimua, na macho yote yatakuwa kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kuona nani ataibuka mshindi katika pambano hili la kuvutia. Je, Simba wataendeleza ubabe wao au Namungo wataandika historia kwa kuwasimamisha Wekundu wa Msimbazi?
Tusubiri kesho, dakika 90 zitaamua.