Klabu ya Simba Sc imepoteza mchezo wa fainali ya pili ya michuano ya kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kukubali sare ya 1-1 dhidi ya Klabu ya Rs Berkane katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa Amaani Visiwani Zanzibar.
Awali katika mchezo wa kwanza uliofanyika katika uwanja wa Manispaa ya mji wa Berkane ilishuhudiwa Simba Sc ikikubali kipigo cha mabao 2-0 na kuwafanya kuwa na kazi ngumu ya kupata sare ya 2-2 au kushinda mabao kuanzia 3-0.
Hata hivyo katika mchezo wa leo kocha Fadlu Davis alimuanzisha Joshua Mutale kama silaha yake ya ushindi ambapo mpaka kufika dakika ya 17 ambapo pasi safi ya Ellie Mpanzu ilifika kwa staa huyo ambaye alipachika bao la kwanza kwa wenyeji.
Hata hivyo bao hilo lilidumu mpaka mapumziko licha ya timu zote kuwa na kosakosa za mara kwa mara ambapo kipindi cha pili Berkane walijitahidi kupooza mchezo kwa pasi fupi fupi na kujiangusha kwa wingi.
Mchezo ulikua mgumu kwa Simba sc baada ya kiungo mkabaji Yousufu Kagoma kupata kadi ya pili ya njano ambayo ilizaa nyekundu na kuwafanya Simba Sc kucheza pungufu kwa dakika takribani 30 za kipindi cha pili.
Licha ya mabadiliko kutoka kwa pande zote mbili bado mechi ilikua ngumu ambapo kocha Fadlu Davis alicheza kamari ngumu akiwaingiza Valentino Nouma na Kibu Dennis akiwatoa Mohammed Hussein na Che Malone Fondoh lengo likiwa ni kuongeza mashambulizi kwake.
Hata hivyo mambo yalibadilika kwa Simba sc dakika ya 90 +3 baada ya Mamadou Sidibe kufunga bao la kusawazisha kutokana na makosa ya kiulinzi ya Simba Sc na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya 1-1 matokeo ambayo yaliwapa kombe Rs Berkane.
Simba sc licha ya kutumia nguvu kubwa kushambulia pia iliathiriwa na maamuzi ya mwamuzi ambaye mara kadhaa alionekana kuwabeba wageni ambao sasa wametwaa kombe hilo kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo.