Historia mpya imeandikwa katika soka la Tanzania baada ya klabu ya Singida Black Stars kukabidhiwa rasmi kiasi cha shilingi milioni tano za motisha maarufu kama Goli la Mama mara ya kwanza tangu ianzishwe.
Tukio hilo lilifanyika leo katika uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam, na kuongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, ambaye aliwakabidhi wachezaji na viongozi wa timu hiyo fedha hizo kama ishara ya pongezi na motisha kwa mafanikio yao.
Singida Black Stars waliweka historia kwa kuifunga Rayon Sports ya Rwanda kwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF Confederation Cup), mchezo ulioibua furaha kwa mashabiki wa timu hiyo na watanzania kwa ujumla.
Bao pekee lililofungwa na Cletous Chama katika mchezo huo liliihakikishia Singida Black Stars nafasi nzuri ya kusonga mbele, huku likiambatana na motisha kubwa kutoka kwa serikali kupitia programu ya Goli la Mama.
Kwa miaka mingi, ilikuwa ni kawaida kuzikuta klabu kongwe na zenye mashabiki wengi nchini, Simba SC na Yanga SC, zikipewa fedha hizo kila mara wanaposhinda michezo yao ya kimataifa.
Motisha hiyo imekuwa sehemu ya hamasa kwa wachezaji na imechangia kuongeza ari ya ushindani kwenye michuano ya Afrika. Hata hivyo, msimu huu Singida Black Stars wamekuwa sehemu ya historia hiyo, jambo linalothibitisha dhamira ya serikali kuunga mkono vilabu vyote vinavyoipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa bila kujali ukubwa wao.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Bw.Gerson Msigwa alipokuwa akikabidhi fedha hizo, alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na vilabu vyote vya Tanzania vinavyoshiriki michuano ya CAF, ili kuongeza heshima na ushindani wa soka la nchi hii. “Tunataka kuona timu zetu zikisonga mbali katika michuano ya Afrika. Leo Singida Black Stars mmeandika historia, na serikali ipo nyuma yenu kuhakikisha mnapata motisha na mazingira bora ya kufanya vizuri,” alisema Msigwa.
Kwa upande wao, viongozi wa Singida Black Stars walieleza furaha yao kwa kupata motisha hiyo kwa mara ya kwanza, wakibainisha kuwa itawaongezea hamasa wachezaji wao kupambana zaidi katika mchezo wa marudiano dhidi ya Rayon Sports na michezo mingine inayofuata. Aidha, waliishukuru serikali kwa kuonyesha upendo sawa kwa klabu zote, jambo linalojenga umoja na mshikamano katika maendeleo ya michezo nchini.
Mashabiki wa soka nchini pia wameipokea hatua hii kwa mikono miwili, wakitambua kuwa sasa mfumo wa motisha unapanuka na kugusa vilabu vipya vinavyopigania heshima ya taifa. Hatua hii inaashiria mwanzo mpya kwa Singida Black Stars, ambao licha ya kuwa wageni katika michuano ya CAF, tayari wameshaweka alama kwa kupata ushindi muhimu na motisha ya kihistoria.
Kwa mara ya kwanza, Singida Black Stars wameonja matunda ya ushindi wa kimataifa kupitia Goli la Mama. Hatua hii si tu inaleta faraja kwa wachezaji na mashabiki wao, bali pia inatuma ujumbe kuwa kila klabu inayoshiriki mashindano ya kimataifa ina nafasi ya kushirikiana na serikali na kujivunia jitihada zao. Huu ni mwanzo wa safari ndefu ya mafanikio, na bila shaka Singida Black Stars sasa wameshaweka wazi kuwa wao ni sehemu ya nguvu mpya za soka la Tanzania barani Afrika.