Dar es Salaam, Oktoba 1, 2025 – Kocha mahiri raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi, amewasili jijini Dar es Salaam tangu jana asubuhi katika kile kinachoelezwa kuwa ni harakati za mwisho za kuhitimisha mazungumzo na moja ya klabu kubwa nchini — Simba SC au Yanga SC.
Nabi, ambaye aliwahi kuwa kwenye benchi la ufundi la Yanga SC na kuifikisha klabu hiyo katika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho CAF msimu wa 2022/23, amerejea nchini kwa wakati ambao vilabu hivyo vikubwa viwili vipo kwenye kipindi kigumu cha maamuzi ya kiufundi.
Kwa upande mmoja, Simba SC ipo katika harakati za kutafuta kocha mkuu mpya baada ya kuachana rasmi na kocha raia wa Afrika kusini Fadlu Davids, ambaye aliondoka baada ya kupata ofa nono kunako klabu ya Raja Casablanca ikiwa na maslahi maradufu kuzidi ya Simba sc.
Kwa upande mwingine, Yanga SC iko katika hali ya sintofahamu chini ya kocha wa sasa Roman Folz, ambaye amekuwa akikosolewa vikali na mashabiki na wadau wa soka kutokana na kushindwa kuipa timu hiyo mwelekeo wa kisoka na uchezaji wa kuvutia licha ya kikosi chake kuwa na nyota wengi wa kimataifa.
Kwa muktadha huo, ujio wa Nasreddine Nabi jijini Dar es Salaam umetengeneza taswira mpya katika anga la soka la Tanzania, huku tetesi zikielekeza kuwa tayari amepanga kukutana na viongozi wa moja ya klabu hizo kuzungumzia mkataba wa kurejea rasmi Ligi Kuu ya NBC.
Yanga au Simba?
Vyanzo vya kuaminika kutoka ndani ya duru za soka vinadai kuwa Nabi huenda akaelekea moja kwa moja Simba SC, klabu ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikimuhusudu kocha huyo kwa falsafa yake ya uchezaji wa kushambulia na nidhamu ya kiufundi. Hata hivyo, pia haijathibitishwa kama Yanga SC imekata tamaa ya kumrudisha mkufunzi huyo aliyeleta mafanikio makubwa kwenye klabu hiyo kabla ya kutimkia Morocco.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Hata hivyo kwa upande wa Simba sc taarifa zinadai kuwa mabosi upande wa mwekezaji wanamtaka kumuajiri kocha huyo lakini kwa upande wa wanachama wanasita kukubaliana na suala hilo kutokana na kuona kuwa kocha huyo ana vinasaba na Yanga sc hivyo wanahisi inaweza kuwa rahisi kuhujumiwa.
Kwa sasa, mashabiki na wachambuzi wa soka wanasubiri kwa hamu kuona uamuzi wa mwisho wa Nabi — je, atavaa tena kijani na manjano, au safari hii atakuwa upande wa pili wa mtaa, akichukua mikoba ya wekundu wa Msimbazi?
Historia Fupi ya Nabi Tanzania
Nasreddine Nabi anasifika kwa kuibadilisha Yanga SC kimfumo na kisaikolojia, na katika kipindi chake cha awali, aliiwezesha klabu hiyo kutwaa mataji ya ndani na kutikisa kwenye anga la Afrika. Anaelezwa kuwa ni kocha mwenye maono makubwa, anayependa soka la kushambulia kwa nidhamu ya hali ya juu.
Kwa hali ilivyo sasa, ujio wa Nabi unaweza kuibua ushindani mpya katika Ligi Kuu ya NBC, iwe atatua Jangwani au Msimbazi.