Winga wa klabu ya Yanga sc Augustine Okrah amefunguka kuhusu kurejea klabuni hapo baada ya kutoka katika majeraha ambayo aliyapata wakati wa kombe la Mapinduzi Visiwani Zanzibar mapema mwaka huu.
Okrah aliumia siku ya mchezo wake wa kwanza klabuni hapo baada ya kugongana na mchezaji wa timu pinzania na kuumia mfupa wa pua hali iliyomlazimu kukaa nje lakini alirejea uwanjani akitoa asisti mbili kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC), ambao chama lake lilishinda 5-0 dhidi ya Polisi Tanzania na juzi kuonyesha kiwango bora alipoingia kipindi cha pili wakati Yanga ikiichakaza CR Belouizdad kwa kichapa mabao 4-0 na kutinga robo fainali.
“Awali nilikuwa na majeraha, hivyo sikupata muda wa kucheza. Ukitoka kwenye majeraha hauwezi kuingia moja kwa moja kikosini, namshukuru Mungu napata nafasi na kucheza na naamini kadri siku zinavyozidi kwenda naimarika zaidi na nitapata muda zaidi wa kucheza na kuonyesha ubora wangu,” alisema Okrah anayevaa kinyago usoni kutokana na jeraha la mishipa ya uso alilolipata.
Okrah aliwahi kuichezea Simba sc ambayo ilimtema na kurudi kwao Ghana alipojiunga na klabu ya Benchem United aliyoifungia mabao tisa katika mechi 16 alizocheza.