Klabu ya Young Africans SC (Yanga) imevunja rasmi mkataba na kocha wake mkuu Roman Folz kufuatia kutoridhishwa na mwenendo wa timu katika michezo ya hivi karibuni, hususan baada ya kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Silver Strikers ya Malawi katika mchezo wa kwanza wa hatua ya pili ya michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika (CAF Champions League) uliochezwa Oktoba 18, 2025, katika uwanja wa Bingu National Stadium nchini Malawi.
Kipigo hicho kimeonekana kuwa kilele cha misururu ya matokeo yasiyoridhisha kwa kocha huyo raia wa Ufaransa, ambaye pia alikosolewa vikali baada ya Yanga kulazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Mbeya City FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC uliofanyika jijini Mbeya wiki zilizopita.
Katika michezo sita iliyopita ya mashindano mbalimbali, Yanga imekuwa ikionyesha kiwango cha chini licha ya kupata ushindi katika baadhi ya mechi, jambo lililowatia wasiwasi viongozi na mashabiki wa klabu hiyo wakubwa nchini.
Kupitia taarifa rasmi kwa umma, uongozi wa Yanga SC umethibitisha kuvunja mkataba na Folz kwa makubaliano ya pande zote mbili, ukisema uamuzi huo ni sehemu ya hatua za kuboresha mwenendo wa timu kuelekea michezo ijayo ya kimataifa na ya ndani.
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa, kwa sasa timu itakuwa chini ya Patrick Mabedi kama kocha wa muda (muangalizi wa kikosi) hadi pale uongozi utakapokamilisha mchakato wa kumpata kocha mpya.
🎯 Usipitwe!
Kuwa wa kwanza kupata habari za moto za michezo nchini Tanzania na duniani kwa ujumla, moja kwa moja kwenye barua pepe yako kutoka SportsLeo Bongo!
- ✅ Matokeo ya mechi
- ✅ Uchambuzi wa kina
- ✅ Habari za ndanii ya timu zako pendwa
✉️ Quality content, no spam. Unsubscribe anytime.
Mabedi anatarajiwa kuiongoza Yanga katika mchezo wa marudiano dhidi ya Silver Strikers utakaochezwa Oktoba 25, 2025, jijini Dar es Salaam, ambapo Yanga italazimika kushinda kwa tofauti ya mabao zaidi ya moja ili kusonga mbele katika michuano hiyo mikubwa ya Afrika.
Uamuzi huu unakuja wakati mashabiki wengi wa Yanga wakitoa maoni yao mitandaoni wakitaka mabadiliko ya haraka ndani ya benchi la ufundi, wakiamini timu hiyo ina wachezaji bora lakini inakosa mbinu na ubunifu unaoendana na uwezo wa kikosi.
Kwa sasa macho yote yameelekezwa kwa Patrick Mabedi kuona kama ataweza kurejesha morali ya timu na kuiwezesha Yanga kupindua matokeo kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Silver Strikers.