Kocha Amani Josiah Aanza Rasmi Kazi Dodoma Jiji FC

Kocha mwenye uzoefu katika soka la Tanzania, Amani Josiah, ameanza rasmi majukumu yake kama Kocha Mkuu wa kikosi cha Dodoma Jiji FC, akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Vicent Mashami ambaye ameripotiwa kutokuwa na sifa za kutimiza majukumu hayo kwa mujibu wa vigezo vya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Josiah, ambaye amewahi kukinoa kikosi cha Geita Gold FC, Biashara United Mara na Tanzania Prisons SC, anatarajiwa kuiongoza Dodoma Jiji katika mchezo wake wa kwanza kesho Oktoba 17, 2025 dhidi ya timu ya Fountain Gate FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ujio wa Josiah umetajwa kuwa ni hatua madhubuti ya uongozi wa Dodoma Jiji FC katika kuhakikisha timu hiyo inajiimarisha kiufundi na kubaki ligi kuu msimu huu, baada ya kuanza msimu kwa matokeo yasiyoridhisha.
Akizungumza kwa kifupi baada ya kuwasili na kuanza rasmi kazi, Kocha Josiah alisema kuwa amepokea nafasi hiyo kwa mikono miwili na anaamini kikosi alichokikuta kina uwezo mkubwa wa kufanya vizuri, endapo kitapewa mbinu sahihi na nidhamu ya mchezo.
“Ninaifahamu Dodoma Jiji, si timu mbovu. Inahitaji kurekebisha baadhi ya maeneo tu na kuongeza morali. Tunaanza na mchezo mgumu dhidi ya Fountain Gate, lakini tutajitahidi kuanza kwa ushindi,” alisema Josiah.
Kwa upande wa uongozi wa klabu hiyo, umetaja sifa na uzoefu wa kocha huyo kuwa moja ya sababu kuu za kumpatia nafasi hiyo, hasa kutokana na mafanikio aliyoyapata katika klabu alizopita. Uongozi umeeleza matumaini yao kuwa Josiah ataleta mabadiliko chanya na kusaidia timu hiyo kupanda kwenye msimamo wa ligi.
Mabosi hao hawakua na ujanja zaidi ya kuajiri kocha mpya baada ya kupigwa faini ya kiasi cha shilingi milioni 15 kutokana na kucheza mechi tatu bila kuwa na kocha mkuu baada ya kocha Vicent Mashami kukosa sifa za kusimama kama kocha mkuu kwa mujibu wa kanuni na taratibu za shirikisho la soka nchini (TFF).
Mchezo dhidi ya Fountain Gate FC unatarajiwa kuwa kipimo kizuri kwa kocha huyo mpya kuelewa kikosi chake, kuona uwezo wa wachezaji wake katika mazingira ya ushindani, na kuanza kujenga mfumo wake wa kiufundi ndani ya klabu.
Wakati mashabiki wa Dodoma Jiji wakisubiri kwa hamu kuona mwanzo mpya chini ya Josiah, ni wazi kuwa kazi kubwa inamngoja kocha huyo, hasa katika kurejesha morali ya timu na kuibadilisha kimtazamo.
Kwa sasa, macho yote yataelekezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kesho, ambako historia mpya itaanza kuandikwa.

