Serengeti Boys Mabingwa Cecafa

Hongera @serengetiboystz kwa kuwa Mabingwa wa CECAFA U17

Serengeti Boys wametangazwa rasmi kuwa wao ndiyo mabwana wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati baada ya kutwaa ubingwa wa michuano ya vijana chini ya miaka 17 ya CECAFA, wakipata ushindi wa kusisimua wa mabao 3–2 dhidi ya mahasimu wao wakubwa, Uganda, kwenye fainali iliyopigwa jioni ya leo Uwanja wa Abebe Bikila, jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Ilikuwa mechi ya kukata na shoka, iliyojaza burudani, presha na vipaji halisi vya soka la vijana. Lakini mwisho kabisa, vijana wa Tanzania walionyesha uthubutu, nidhamu na njaa ya ubingwa na walichokipata walikistahili.

Mbegelendi awa mwiba mchungu kwa Uganda

Bohari ya furaha ya Watanzania leo inapaswa kufunguliwa kwa jina moja tu Razak Juma Mbegelendi. Kijana huyu kutoka mtaa mwenye kipaji alibeba mzigo mzima wa ushambuliaji wa Serengeti Boys, akipiga mabao mawili dakika ya 6 na 30, na kuwafanya mashabiki wa Tanzania waanze kuamini mapema kuwa taji linaweza kurudi nyumbani.

Serengeti Boys Mabingwa Cecafa-www.sportsleo.co.tz

Bao lake la kwanza lilikuwa la ustadi wa hali ya juu, akimalizia mpira wa krosi kabla ya kuweka goli kambani. Uganda walijibu mapigo kupitia Thomas Ogema dakika ya 13, lakini Serengeti Boys hawakutetereka badala yake walizidisha kasi na kumiliki mchezo.

Kabla hata Uganda hawajapumua, kijana mwingine mwenye kipaji kinachochanua, Luqman Mbalasalu, aliandika bao la tatu dakika ya 45, bao lililowamaliza kabisa Waganda kipindi cha kwanza na kuweka fainali upande wa Tanzania.

Uganda walijaribu, lakini moto wa Serengeti Boys ulikuwa mkubwa

Kipindi cha pili Uganda walirudi na ari mpya, wakipambana kutafuta mabao ya kurejea mchezoni. Waliongeza kasi, wakacheza soka la nguvu, lakini ukuta wa Serengeti Boys ukiongozwa na vijana jasiri uliwazuia mara nyingi.

Bao la pili la Uganda lilikuja dakika za nyongeza kupitia Brian Olwa dakika ya 90’+6, lakini lilikuwa ni namba tu kwenye takwimu hakukuwa na muda wa kuwaumiza Serengeti Boys waliokuwa tayari wameshachora historia.

Baada ya kipyenga cha mwisho, wachezaji wa Serengeti Boys walikimbiana, wakashangilia kwa nguvu wakiwa wamejifunika bendera za Taifa, wakikumbatiana na benchi la ufundi. Picha zao zilisheheni tabasamu, machozi ya furaha na hisia za kujivunia kazi kubwa waliyofanya.

Serengeti Boys Mabingwa Cecafa-www.sportsleo.co.tz

Ethiopia wazima Kenya, wapata nafasi Morocco

Katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu mapema leo, wenyeji Ethiopia waliwafanyia Kenya kile ambacho hakikutegemewa na mashabiki wengi—kuwapiga 3–0 bila huruma. Mabao hayo yalifungwa na Dawit Kassaw (67’), Binyam Abrha (79’) na Biruk Eyirachew (90’+3).

Ushindi huo uliwapa Ethiopia nafasi ya tatu, ikiwa ni mafanikio makubwa kwa timu ambayo ilionekana kuboresha mchezo kadri michuano ilivyokuwa ikiendelea.

Nani wanaenda Morocco?

Licha ya kupoteza taji, Uganda ambao walikuwa mabingwa watetezi, hawajaondoka mikono mitupu. Kwa mujibu wa kanuni za mashindano, Tanzania, Uganda na Ethiopia wenyeji wa fainali ndogo waneungana kuwakilisha CECAFA kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-17) zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.

Hii inamaanisha Serengeti Boys wanaongeza ukurasa mwingine kwenye historia yao, sio tu kwa kutwaa ubingwa bali pia kwa kufuzu mashindano ya bara ambako wanatarajiwa kupeperusha bendera ya Tanzania kwa uzito na heshima.

Ushindi wenye thamani kubwa

Ushindi huu unakuja katika kipindi ambacho Tanzania imewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye soka la vijana. Ndiyo maana mafanikio haya yamesifiwa na wadau kama ishara ya kizazi kipya chenye matumaini mapya.

Wachambuzi wa soka wanasema Serengeti Boys wameonyesha kitu ambacho kwa muda kimekosa kuonekana kwenye timu za vijana nidhamu ya kiufundi, uwezo binafsi wa wachezaji, na uwezo wa benchi la ufundi kusoma mchezo.

Kwa sasa, kinachofuata ni maandalizi ya safari kuelekea Morocco, safari ambayo wadau wengi wanaitazama kama fursa ya Tanzania kuonyesha vipaji vyake kwenye anga pana zaidi la Afrika.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks