Dube Atoboa Afcon 2025

Kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya Zimbabwe The Warriors, Marian “Mario” Marinică, ametangaza rasmi kikosi chake kitakachoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, zitakazoanza kutimua vumbi nchini Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026. Tangazo hilo limeibua hisia mpya miongoni mwa mashabiki wa soka wa Zimbabwe na ukanda wa Kusini mwa Afrika, kwani linaonekana kuleta matumaini mapya kwa taifa hilo ambalo limekuwa likihangaika kurejea kwenye ramani ya soka barani.
Kikosi hicho, ambacho mara ya mwisho kushiriki AFCON kilikuwa kikikumbwa na mabadiliko ya kiutawala na changamoto za ndani ya Shirikisho la Soka Zimbabwe (ZIFA), safari hii kinaonekana kuundwa kwa umakini mkubwa na mkono wa kocha Marinică ambaye amekuwa akisisitiza nidhamu, kasi na uwekezaji kwenye wachezaji wanaocheza nje ya nchi na wale wanaofanya vizuri katika ligi za Afrika Mashariki na Kusini.

Miongoni mwa majina yaliyoleta shangwe kubwa ni lile la mshambuliaji wa Yanga SC, Prince Mpumelelo Dube, ambaye amekuwa katika kiwango bora msimu huu akiwa na klabu yake hiyo ya Tanzania. Dube, ambaye amewahi kupambana na majeraha ya mara kwa mara, amerejea kwa nguvu mpya na mchango wake katika kikosi cha Yanga umeonyesha wazi kwa nini Marinică hampuuzi katika mipango yake. Mashabiki wengi wa Zimbabwe wameonyesha furaha kuona jina lake likirejea kwenye orodha ya wachezaji watakaopambana kupeperusha bendera ya taifa.
Katika AFCON 2025, The Warriors wamepangwa Kundi B, kundi linalotajwa na wachambuzi wengi kuwa miongoni mwa magumu zaidi. Wanakutana na Afrika Kusini (Bafana Bafana), Misri (The Pharaohs) na Angola (Palancas Negras). Kundi lenye mabingwa wa kihistoria, timu zenye uzoefu mkubwa barani Afrika, na zilizowahi kufanya maajabu katika michuano ya kimataifa. Kwa upande wa Zimbabwe, wengi wanaona hii ni fursa ya pekee kuonyesha kuwa kizazi kipya cha wachezaji kinaweza kupambana na vigogo hao bila kuogopa majina yao makubwa.

Kocha Marinică, akizungumza mara baada ya kutangaza kikosi hicho, alisema kuwa “Tunakijenga kikosi kinachochezewa kwa moyo, kazi na nidhamu. Zimbabwe ina vipaji vingi, lakini tunahitaji timu ambayo itapambana kwa dakika 90 bila kukata tamaa. Tunaheshimu wapinzani wetu lakini hatuwaogopi.”
Katika safu ya ulinzi, Marinică amejumuisha mchezaji mkongwe anayecheza Afrika Kusini, huku kiungo kiongozi kutoka ligi ya Zambia akikamilisha orodha ya wachezaji wanaotazamwa kufanya vizuri katikati ya uwanja. Safu ya ushambuliaji inayomjumuisha Prince Dube, inayosaidiwa na wachezaji wawili wanaocheza Ulaya Mashariki, imeongeza matumaini kuwa Zimbabwe inaweza kufunga mabao muhimu katika kundi linalotarajiwa kuwa na ushindani mkali.
Mashabiki wamepokea tangazo hilo kwa hisia kali. Wengi wanaamini huu ni mwanya wa kurejesha hadhi ya The Warriors baada ya misukosuko ya miaka ya karibuni. Mitandaoni, wafuasi wa soka wamekuwa wakimpa sapo Kocha Marinică kwa kufanya maamuzi “yenye macho ya kitaalamu”, ikiwemo kumrejesha Dube ambaye wengi walisema ni lazima awe sehemu ya kikosi hicho.
Huku maandalizi yakiendelea, kikosi kinatarajiwa kuingia kambini katikati ya mwa mwezi Desemba jijini Harare kabla ya kuelekea Morocco kwa mechi za kirafiki mbili za mwisho. Kocha ametahadharisha kuwa ushindani kwenye nafasi za kucheza bado uko wazi, na kila mchezaji atalazimika kupambana kuthibitisha ubora wake.
Kwa sasa, macho yote nchini Zimbabwe na Afrika Mashariki yameelekezwa kwa The Warriors. Je, wataandika historia mpya katika AFCON 2025? Je, kizazi cha wakina Prince Dube kitaweza kuikomboa Zimbabwe na kuivusha hatua za makundi?Tusubiri tuone maana wahenga walisema tusiandikie mate wakati wino upo.
