Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma imesema kuwa haiwezi kuingilia mgogoro unaoendelea kuhusu mechi ya Darby kati ya Simba na Yanga kutokana na kuwepo mamlaka inayosimamia soka nchini ambayo ni Shirikisho la soka (TFF)
Mwinjuma amesema hayo bungeni jijini Dodoma mapema hii leo wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Jimbo la makete Mh.Festo Sanga aliyetaka kujua hatima ya mvutano wa timu mbili za Simba sc na Yanga sc pamoja na TFF.
“Shughuli za mpira wa mguu una mamlaka zake za kimataifa na za kitaifa na tumekuwa tukisisitizwa mara kwa mara serikali kutoingilia moja kwa moja uendeshaji wa shughuli hizo ili kuepuka kuja kufungiwa nna Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa nyakati hizi hata kitakwimu nchi yetu inafanya vizuri katika uendeshaji wa shughuli za mpira wa mguu”,Alisema Mh.Hamis Mwinjuma Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo mbele ya wabunge bungeni humo.
“Kuhusu mchezo anaousema serikali inafuatilia kwa karibu jinsi ambavyo mgogoro huu unaendelea kutatuliwa lakini huku tukijaribu kwa kiwango kikubwa kutoingilia moja kwa moja maamuzi ya TFF na Bodi ya ligi” alimalizia kusema na kuamsha makofi kwa baadhi ya wabunge.
Mpaka sasa hali ya soka nchini imekua na sintofahamu kufuatia mgogoro huo ulioanza tangu machi 8 2025 baada ya klabu ya Simba Sc kugomea mchezo baina yake na Yanga sc baada ya siku moja kabla kuzuiwa kufanya mazoezi katika uwanja wa mechi kwa mujibu wa kanuni.