Home Makala Yanga Sc Kuanza Safari Yake Ya Ligi Kuu Dhidi Ya Pamba FC Leo Usiku

Yanga Sc Kuanza Safari Yake Ya Ligi Kuu Dhidi Ya Pamba FC Leo Usiku

by Dennis Msotwa
0 comments

Dar es Salaam, Septemba 24, 2025

Klabu ya Yanga SC leo usiku saa moja itashuka dimbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, kwa mara ya kwanza msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kumenyana na kikosi cha Pamba Jiji FC kutoka Mwanza, katika mchezo unaotarajiwa kuwa wa kuvutia na wenye ushindani mkubwa.

Kwa upande wa Yanga SC, huu utakuwa mchezo wao wa kwanza rasmi katika ligi baada ya kutoka kwenye maandalizi ya msimu mpya yaliyofanyika ndani nchi wakianzia katika uwanja wa Kmc na kisha Avic Town Kigamboji Dar es salaam. Huku ikiwa na kikosi kipana kilichoboreshwa kwa kusajili wachezaji wapya, Yanga SC inatazamiwa kuanza msimu kwa kishindo mbele ya mashabiki wake wengi watakaofurika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

banner

Kocha mkuu wa Yanga SC, Roman Folz, amesema kuwa atapanga kikosi chake kutokana na kile alichokiona katika mazoezi ya timu hiyo kwa siku kadhaa zilizopita. “Msimu huu kila mechi tunahitaji kupata alama tatu kila mechi. Yanga ni timu kubwa, malengo yetu ni kutwaa ubingwa wa ligi. Tunawachezaji bora sana na kikosi kipana. Kila Mchezaji kwangu ni muhimu. Unaweza kumuona mchezaji mmoja leo, mchezo unaokuja usimuone. Nitatoa nafasi kwa kila mchezaji kulingana na anavyojituma” alisema Folz kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana. “Tunawaheshimu Pamba, lakini sisi ni Yanga, tupo tayari kuanza kampeni yetu vizuri.”

Kwa upande mwingine, hii itakuwa mechi ya pili kwa Pamba Jiji FC ambao walipanda daraja msimu uliopita. Katika mchezo wao wa kwanza, waliibuka na sare ya bao 1-1 dhidi ya Namungo FC ugenini mjini Ruangwa, matokeo ambayo yaliwapa matumaini makubwa kuhimili ushindani wa ligi.

Kocha wa Pamba Jiji FC, Francis Baraza, amezua mjadala baada ya kutoa kauli ya kushangaza akisema kuwa “kucheza dhidi ya Yanga SC ni rahisi kuliko kucheza na Namungo FC.” Baraza alisema kuwa licha ya ukubwa wa Yanga, wanajua wanavyocheza na wamejiandaa kuwakabili tofauti na namna walivyohitaji kujipanga kwa Namungo, ambao, kwa mujibu wake, walikuwa wagumu zaidi kubashiri mitindo yao ya uchezaji.

“Hatuwaogopi Yanga. Tunawaheshimu kwa mafanikio yao lakini hatuendi kucheza kwa hofu. Tunajua udhaifu na nguvu zao. Tunataka kuonyesha kuwa Pamba ipo Ligi Kuu kwa sababu sahihi,” alisema Baraza.

Mchezo huu pia utakuwa kipimo kikubwa kwa Pamba kuona kama wanaweza kuhimili presha ya kucheza mbele ya umati mkubwa wa mashabiki wa soka, hasa kutoka klabu kubwa kama Yanga SC. Kwa upande wa Yanga, huu ni muda wa kuonyesha dhamira yao ya kutetea ubingwa walioupata msimu uliopita kwa kishindo.

Tayari maandalizi yamekamilika, tiketi zimeuzwa kwa wingi na mashabiki wa Yanga wanatazamiwa kuujaza Uwanja wa Mkapa kwa lengo la kuisapoti timu yao kipenzi. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limethibitisha kuwa maandalizi ya kiusalama na uendeshaji wa mchezo huo yapo katika viwango vya juu, huku refa aliyepangwa pia akiwa ni mzoefu kutoka kundi la waamuzi wa kati waliothibitishwa kwa msimu huu.

Kwa mashabiki na wadau wa soka nchini, mchezo huu unatarajiwa kuwa mwanzo mzuri wa burudani ya soka msimu wa 2025/2026, huku macho yote yakielekezwa kwa mabingwa watetezi, Yanga SC, kuona kama wataanza msimu kwa kishindo au kama kikosi kipya cha Pamba Jiji FC kitaibuka na kejeli ya msimu mapema kabisa.

You may also like

Leave a Comment

Sportsleo Bongo ni tovuti ya kwanza na bora zaidi ya michezo nchini Tanzania, ikileta habari kwa Kiswahili, matokeo ya moja kwa moja, tetesi, na taarifa muhimu kuhusu soka, ndondi, riadha na michezo mingine ndani na nje ya Tanzania.

Edtior's Picks

Latest Articles

Sportsleo Bongo Developed and designed by Mediapix Limited