Klabu ya Yanga sc itavaana na Mamelod Sundowns katika mchezo wa hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa barani Afrika baada ya droo iliyofanyika jioni ya leo jijini Cairo nchini Misri yalipo makao makuu ya Shirikisho la soka barani Afrika (Caf).
Yanga sc kwa mujibu wa droo itaanzia nyumbani kati ya Machi 29-31 mwaka huu mchezo ambao utafanyika katika uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es salaam na marudiano yatakua nchini Afrika ya kusini kati ya Aprili 5-7 ambapo mshindi wa jumla atafuzu hatua ya nusu fainali ambapo atakutana na mshindi kati ya Asec Mimosa na Esperance de Tunis.
Yanga sc watakua na kazi ya ziada kuwafunga Mamelod kutokana na ukweli kwamba timu hiyo kwa sasa ni moja ya timu bora na ngumu barani Afrika huku ikiwa na kikosi cha gharama zaidi ambapo kuna mastaa waliosajili kwa mabilioni ya pesa tofauti na Yanga sc.
Awali malengo ya Yanga sc yalikua ni kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo ambayo hawakua wamefuzu kwa takribani miaka 25 na sasa wapo hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ambapo kufuzu nusu fainali inaonekana ni ndoto ngumu kwa sasa.
Katika michuano ya Caf mara ya mwisho Mamelod Sundowns ilipoteza mchezo 2/12/23 ambapo ilifungwa na Tp Mazembe ugenini kwa 1-0 ambapo tangu hapo haijapoteza katika mechi za ndani na nje ya Afrika Kusini.