Gamondi Aanza Kazi Stars Akiivaa Kuwait

Kocha wa Taifa Stars Miguel Gamondi na Kocha Msaidizi Ahmad Ally wakijadiliana wakati wa mazoezi

Safari mpya ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeanza rasmi chini ya uongozi wa Kocha Mkuu Miguel Ángel Gamondi na msaidizi wake Ahmad Ally, baada ya wawili hao kuanza rasmi mazoezi na kikosi hicho leo, Novemba 10, 2025, jijini Dar es Salaam.

Gamondi, ambaye alitangazwa rasmi kuchukua mikoba ya Hemed Morocco mwezi uliopita, amesisitiza kuwa huu ni mwanzo mpya wa enzi ya soka la kisasa ndani ya Stars, akiahidi timu yenye nidhamu, ubunifu na uwezo wa kupambana na timu yoyote barani Afrika.

Kibarua cha kwanza cha benchi jipya la ufundi kitakuwa ni mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Kuwait, unaotarajiwa kuchezwa Novemba 14, 2025, mjini Cairo, Misri. Mchezo huo unatajwa kuwa kipimo muhimu kwa Gamondi kuelekea kampeni za kufuzu Kombe la Dunia na mashindano ya AFCON yajayo.

Katika mazoezi ya kwanza yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Gymkana jijini Dar es salaam, Gamondi aliweka mkazo katika mbinu za pasi za haraka, umiliki wa mpira, na mipangilio ya kiufundi, huku wachezaji wakionekana wenye ari kubwa kuonyesha uwezo wao mbele ya benchi jipya la ufundi.

Gamondi Aanza Kazi Stars Akiivaa Kuwait-www.sportsleo.co.tz

Kikosi hicho kimejumuisha nyota wanaocheza ndani na nje ya nchi, lakini gumzo kubwa limekuwa ni wito wa wachezaji wapya, akiwemo Idd Seleman wa Azam FC na Kelvin Nashon, nyota chipukizi anayeng’ara Ligi Kuu msimu huu akicheza kwa mkopo katika klabu ya Pamba Jiji Fc. Wachezaji hao wameitwa kwa mara ya kwanza chini ya Gamondi, hatua inayotafsiriwa kama ishara ya kocha huyo kuanza upya kwa kutafuta damu changa yenye njaa ya mafanikio.

Akizungumza baada ya mazoezi, Gamondi alisema anafurahia mazingira ya kikosi na ari waliyoonyesha wachezaji, akisisitiza kuwa mechi dhidi ya Kuwait itampa nafasi ya kuona mapungufu na nguvu za wachezaji wake kabla ya mechi ngumu zijazo.

“Ni muhimu kuanza kwa mtazamo sahihi. Mechi dhidi ya Kuwait si tu ya kirafiki, bali ni kipimo cha kuelewa uwezo wa timu yangu. Tunahitaji kujenga timu imara, inayocheza kwa maelewano na nidhamu kubwa,” alisema Gamondi.

Kwa upande wake, Ahmad Ally, ambaye ni miongoni mwa makocha vijana wanaopanda kwa kasi nchini, alisema anajivunia kuwa sehemu ya benchi jipya na atatumia nafasi hiyo kuhakikisha Stars inarejea kwenye ubora wake wa zamani.

“Kuwa sehemu ya timu ya taifa ni heshima kubwa. Tumeanza kazi kwa nguvu, tunataka kuona Taifa Stars inakuwa timu ya ushindani siyo tu barani Afrika bali pia kimataifa,” alisema Ahmad.

Katika kambi hiyo, nyota wengine walioungana na timu ni pamoja na Novatus Dismas, Dickson Job,Paschal Msindo na Bakari Mwamnyeto, huku baadhi ya wachezaji wanaocheza nje ya nchi wakitarajiwa kuwasili kesho.

Mchezo dhidi ya Kuwait unatajwa kuwa na umuhimu mkubwa kwa TFF na mashabiki wa Stars, kwani utatoa taswira ya mabadiliko yanayoletwa na Gamondi. Mechi hiyo pia inatarajiwa kumsaidia kocha huyo kutengeneza muunganiko sahihi kati ya wachezaji wenye uzoefu na kizazi kipya cha soka cha Tanzania.

TFF imeeleza kuwa maandalizi yote yamekamilika, na Stars itasafiri kuelekea Cairo Alhamisi usiku kwa ndege maalum.

Mashabiki wengi wamepokea kwa matumaini makubwa uteuzi wa Gamondi, wakiamini uzoefu wake alioupata akiwa na klabu kama Mamelodi Sundowns, USM Alger, na Yanga sc SC, utasaidia kuinua hadhi ya timu ya taifa.

Kwa upande mwingine, wadau wa soka wamesema ujio wa Ahmad Ally, kocha anayefahamika kwa kazi nzuri katika kukuza vipaji ndani ya nchi, ni faida kwa Stars kwani ataleta mawasiliano mazuri kati ya wachezaji wa ndani na benchi la ufundi.

Kambi ya Taifa Stars imeanza kwa ari kubwa na hamasa, huku kila mchezaji akipigania nafasi yake kwenye kikosi cha kwanza. Mashabiki sasa wanasubiri kuona matokeo ya kazi ya Gamondi na Ahmad katika mchezo wa kwanza dhidi ya Kuwait, mechi itakayotoa dira ya safari mpya ya Stars chini ya uongozi wa kocha huyo wa Kiargentina.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks