Wawili Kuamua Hatma ya Yao Yanga Sc


Wakati dirisha dogo la usajili nchini Tanzania likielekea kufunguliwa, ndani ya klabu ya Yanga sc wenyeji wa mitaa ya Twiga na Jangwani hali si shwari. Si kwa presha ya mechi tu, bali kwa suala moja linalotikisa meza ya usajili pale makao makuu ya klabu ikiwa ni mustakabali wa beki wa kulia raia wa Ivory Coast, Yao Kouassi.
Beki huyo, ambaye msimu huu haukuanza naye kutokana na majeraha ya muda mrefu, amerejea uwanjani na kuanza kufanya mazoezi mepesi. Hilo peke yake limeshawasha mjadala mzito miongoni mwa benchi la ufundi la Yanga na mashabiki, wakitaka kujua je, Yao anarudi kwenye usajili wa klabu, au safari yake inakwenda kubadilika?

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na uongozi, Yanga imekabidhi jukumu hilo kwa watu wawili tu ambao ni Kocha Mkuu, Pedro Gonçalves, na Kocha wa Utimamu wa Mwili, Chyna Mokaila. Hawa wawili, kwa kauli moja au tofauti, ndiyo watakaoamua hatima ya mchezaji huyo ndani ya dirisha dogo.
Yao Hayumo Kwenye Orodha ya Wageni 12 Lakini Mlango Bado Upo Wazi
Katika dirisha kubwa la usajili lililopita, Yanga ilisajili jumla ya wachezaji 12 wa kigeni, orodha ambayo haikumjumuisha Yao. Klabu iliamua kwanza kumtibu,kisha kumpa muda wa kupona (rehabilitation) na kumfanya afanye programu maalum nje ya kikosi cha kawaida, ikiamini bado anaweza kuwa msaada pindi atakaporejea kwenye ubora wake.

Kwa mujibu wa kanuni, Yanga inaweza kumuingiza Yao kwenye usajili wa dirisha dogo iwapo itapunguza mchezaji mmoja wa kigeni. Hapo ndipo shughuli inapoanza, kwani ni nani aondoke ili nafasi yake imwachie Yao? Hili ndilo gumzo linalokwenda kulipuka mitaani, mitandao ya kijamii na hata vijiwe vya kahawa jijini Dar.
Kamwe Afunguka Kila Kitu Kipo kwa Ripoti ya Chyna na Uamuzi wa Pedro
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe, kwa mara nyingine amekuwa mstari wa mbele kutoa ufafanuzi. Kwa sauti iliyojaa umakini, alisema:
“Kwasi Attohoula Yao, tunachosubiri sasa hivi ni ripoti kutoka kwa kocha wa utimamu wa mwili. Mchezaji ambaye ametoka kwenye majeraha ni ngumu mno kumkadiria kwamba akishapona atarudi. Ikituambia kwamba mchezaji huyu amekamilika kwa asilimia mia, mwalimu atakuwa na namna yake ya kumchunguza Yao kuangalia ubora wake umefika wapi.”
Akiongeza, Kamwe alisema hatua ya pili iko mikononi mwa Pedro “Halafu yeye anatugeia sisi mapendekezo yake kwamba sasa hivi mnaweza kumuingiza kwenye usajili, nitamtumia. Amefika kwenye kiwango anachohitaji yeye tumuingize kwenye usajili au tumuache aendelee kufanya naye mazoezi au tumtoe kwa mkopo apate muda wa kucheza. Yote yanaweza kutokea hayo.”
Kwa hivyo kwa tafsiri nyepesi ni kwamba ripoti ya Chyna itaamua ‘yuko fiti kiasi gani’, na Pedro ataamua ‘anafaa kiasi gani’ na hivyo hao wawili wataamua abaki ama aondoke Yanga sc.
Kwanini Yao Amezua Mjadala Mkubwa?
Kabla ya kuingia kwenye majeraha, Yao alishawahi kutazamwa kama beki wa kulia mwenye uwezo mkubwa, nguvu, kasi na uwezo wa kupandisha mashambulizi. Alikuwa moja ya “project players” wa Yanga waliokua wanatarajiwa kufanya makubwa zaidi.
Mara kadhaa, benchi la ufundi liliwahi kuhimiza kuwa Yao anaweza kuwa msaada kwa muda mrefu akicheza sambamba na mastaa kama Aucho,Dickson Job na Pacome Zouzoua. Hata hivyo, majeraha ndiyo yaliyokatisha safari yake na kumtoa kwenye hesabu za msimu huu.
Kwa sasa, kutokana na presha ya mechi za Ligi Kuu na CAF Champions League, Yanga wanatafuta depth ya kutosha kwenye nafasi hiyo. Yao akirudi kwenye ubora wake, anaweza kuiongezea timu ushindani na upana wa kikosi.
Changamoto Kubwa Nani Ataondoka Ili Yao Aingie?
Hii ndiyo pointi ngumu kwa sababu nafasi mojawapo lazima itoke kwa mchezaji wa kigeni ili kukidhi matakwa ya wachezaji 12 wa kigeni hasa katika ligi kuu japo kimataifa kanuni bado inaruhusu zaidi ya wachezaji 12.
Kwa ratiba ya misimu iliyopita, mara nyingi Yanga wamekuwa wakifanya maamuzi mazito ya kuachana na mchezaji wa nje ambaye hajatimiza matarajio. Lakini safari hii, karibu wageni wote wa kikosi wanaonekana kutumika mara kwa mara na kuaminiwa na benchi la ufundi.Hivyo, uamuzi wa kuachana na mmoja wao si mwepesi na unaweza kuibua mjadala mpya zaidi.
Mambo Matatu Yatakayoamua Hatima ya Yao
1. Hali ya kiafya na utimamu wake
Chyna Mokaila ndiye mtu muhimu hapa. Atatoa ripoti kuhusu uwezo na uthabiti wa misuli, hatari ya kurejea kwenye majeraha na muda anaoweza kutumika uwanjani bila hatari.
2. Mahitaji ya kiufundi ya Pedro
Pedro anataka nini kwenye mfumo wake? Je, anahitaji beki wa kulia anayepanda na kushuka kwa kasi au anahitaji mtu wa nidhamu ya ulinzi kwanza? Kama Yao hana sifa anazoangalia, nafasi yake itakuwa finyu.
3. Kasi ya kurejea kwenye ubora wa kitambo
Yanga wanapambana kwenye mashindano mbalimbali. Hawana muda wa kusubiri miezi mingine miwili au mitatu kumsubiri mchezaji kuwa “full sharp”. Wanaweza tu kumrudisha kama yuko tayari kucheza mara moja.
Yote Yafunguka Dirisha Dogo Likifunguliwa
Hali ya Yao itajulikana ndani ya wiki chache zijazo. Kwa sasa, mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona kama kijana huyo wa Ivory Coast atarejea rasmi kambini kama sehemu ya masplan ya Yanga au kama atachukuliwa kama “project” ya muda mrefu ya kupewa muda wa mkopo ili apate muda wa kucheza ikizingatiwa sasa Israel Mwenda anafanya vizuri kwenye nafasi hiyo.
