Kapombe Atikisa Afrika

567498567 18514561117071034 6311784779139993465 n

Nahodha wa klabu ya Simba SC, Shomari Kapombe, ameandika historia mpya katika soka la Tanzania baada ya kutajwa rasmi kwenye orodha ya wachezaji 10 wanaowania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka 2025 (CAF – Home Based Player of the Year), inayotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

Kapombe, ambaye amekuwa nguzo muhimu ndani ya kikosi cha Simba na Timu ya Taifa ya Tanzania ”Taifa Stars, ameingia kwenye orodha hiyo ya heshima kubwa sambamba na mastaa wakubwa wa soka barani Afrika akiwemo mshambuliaji hatari wa zamani wa Yanga SC, Fiston Kalala Mayele, ambaye kwa sasa anakipiga kwenye klabu ya Pyramids FC ya Misri.

Ni wazi kuwa hii ni habari njema kwa mashabiki wa soka nchini, hasa wa klabu ya Simba Sc, wanaoona uamuzi huu wa CAF kama uthibitisho wa ubora na uthabiti wa Kapombe ndani na nje ya uwanja.

Kapombe Atikisa Afrika-www.sportsleo.co.tz

HESHIMA KUBWA KWA SIMBA NA TANZANIA

Kapombe anakuwa Mtanzania pekee kuingia katika orodha hiyo mwaka huu  jambo linaloonyesha jinsi alivyopiga hatua kubwa kimataifa. Nahodha huyo mwenye uzoefu wa miaka mingi kwenye soka la Tanzania ameendelea kuwa kiongozi wa mfano, akiwa mhimili wa Simba SC kwenye safu ya ulinzi.

Kwa misimu miwili mfululizo, Kapombe amekuwa mchezaji wa kuigwa kutokana na nidhamu yake, maamuzi sahihi na namna anavyoliongoza jeshi wekundu wa Msimbazi ndani ya uwanja. Wataalamu wa soka wameeleza kuwa uteuzi wake kwenye tuzo hii ni matokeo ya kazi kubwa anayofanya kimyakimya.

“Kapombe ni mchezaji anayecheza kwa akili, anajua wakati gani aende mbele na wakati gani abakie kulinda. CAF hawakukosea kumweka kwenye orodha hii,” alisema mchambuzi wa soka, ambaye hakutaka jina lake liwekwe wazi.

MASTAA WAKUBWA WAMEMZUNGUKA

Katika orodha hiyo, Kapombe anakutana na nyota 9 waliotamba kwenye vilabu mbalimbali barani Afrika, akiwemo Fiston Kalala Mayele (Pyramids FC, Misri) ambaye bado ana kumbukumbu kali kwa mashabiki wa Tanzania kutokana na mchango wake alipokuwa Yanga SC.

Wengine waliotajwa ni Ismail Belkacemi wa Al Ahli Libya, Ibrahim Blati Touré wa Pyramids FC, Issoufou Dayo (zamani wa RS Berkane, sasa Umm Salal SC – Qatar), na Emam Ashour wa Al Ahly ya Misri.

Listi hiyo pia inajumuisha nyota mwingine wa zamani wa Pyramids FC, Ibrahim Adel, ambaye sasa anakipiga Saudi Arabia kwenye klabu ya Al Jazeera FC, pamoja na Mohamed Hrimat (AS FAR Rabat), Mohamed Chibi (Pyramids FC), na Oussama Lamlioui (RS Berkane).

Ni orodha nzito yenye majina makubwa, lakini Kapombe anaingia akiwa na rekodi safi ya ubora na uongozi ndani ya uwanja – jambo linalompa nafasi ya kushindana vikali katika kinyang’anyiro hiki cha heshima.

Kapombe Atikisa Afrika-www.sportsleo.co.tz

KAPOMBE: “NI HESHIMA KUBWA KWA TAIFA LANGU”

Akizungumza kwa kifupi baada ya taarifa hizo kuthibitishwa na CAF, Kapombe alisema uteuzi huo ni matokeo ya bidii na imani ya mashabiki wa Simba pamoja na Watanzania kwa ujumla.

“Nimepokea taarifa hii kwa furaha kubwa. Ni heshima kwa klabu yangu, kwa wachezaji wenzangu, na kwa Tanzania yote. Nitazidi kupambana ili kuipeperusha bendera yetu juu zaidi,” alisema Kapombe kwa unyenyekevu.

Nahodha huyo aliongeza kuwa safari yake bado haijaisha, kwani anataka kuona wachezaji wengine wa Tanzania wakifika viwango vya kimataifa kama hivi.

Kapombe Atikisa Afrika-www.sportsleo.co.tz

WATANZANIA WAPONGEZA, SIMBA YATOA TAARIFA RASMI

Kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii ya klabu ya Simba SC hawakusita kumpongeza nahodha wao huyo ambapo katika mtandao wa instagram klabu hiyo iliweka chapisho linalosomeka;

”Nahodha wetu Shomari Kapombe ametajwa kuwa mmoja wa wachezaji ambao wanawania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka anayecheza ndani ya bara la Afrika.”

MWISHO WAKE

Kwa uteuzi huu, Shomari Kapombe ameweka jina lake kwenye ukurasa wa heshima wa wanasoka bora Afrika wanaocheza ligi za ndani. Ni hatua kubwa si kwa yeye binafsi tu, bali kwa Simba SC na soka la Tanzania kwa ujumla.

Mashabiki sasa wanasubiri kuona kama atavuka hatua ya 10 bora na kufika kwenye tatu bora  hatua ambayo inaweza kuweka jina lake kwenye orodha ya mastaa waliowahi kung’ara barani Afrika.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks