Kiungo mshambuliaji wa klabu ya Dodoma Jiji Ibrahim Ajibu amesimamishwa na uongozi wa klabu hiyo sambamba na golikipa wa klabu hiyo Allan Ngereka kwa utovu wa nidhamu kambini.
Kwa mujibu wa afisa habari wa klabu hiyo Moses Mpunga amethibitisha kuwa wachezaji hao wawili wa klabu hiyo yenye makazi yake jijini Dodoma wamesimamishwa kwa matukio ya utovu wa nidhamu.
“Sisi kama klabu moja ya misingi yetu ni nidhamu kwahiyo kwa namna moja au nyingine tukiona viashiria vya utovu wa nidhamu au mtu kwenda kinyume na katiba na sheria ambazo tumewekeana basi zipo adhabu ambazo tumekubaliana basi tunatekeleza hizo”.Alisema Afisa habari huyo wakati akizungumza na mwandishi wetu.
“Generally tunasema ni utovu wa nidhamu hatuwezi kusema kitu gani walichofanya unaweza ukamdhalilisha huyo mtu na wewe ukawa sehemu ya huo utovu wa nidhamu, Waliosimamishwa ni Ibrahim Ajibu na golikipa Allain Ngeleka”.
Alipoulizwa kuwa haoni kama wachezaji hao wana msaada kwa mechi zijazo za klabu ambapo wanakutana na Yanga sc katika mchezo unaofuatia wa ligi kuu alisema kuwa “hata kama tungekuwa tunakutana na Real Madrid utovu wa nidhamu sisi kwetu mara kumi tupoteze wachezaji wote lakini Kila mchezaji tumsimamishe kama ana utovu wa nidhamu kuliko kuvumilia tabia ambazo sio sahihi kwenye jamii yetu ambayo tumejiwekea eti kisa tu anaweza kutusaidia kwenye mechi fulani hicho kitu kwetu sio sehemu ya taasisi yetu”.Alisema kwa uchungu Afisa habari huyo.
Dodoma jiji Fc kesho itakutana na Yanga sc katika mchezo wa mwisho wa ligi kuu ya soka ya Nbc ambao utafanyika katika uwanja wa Amaani Visiwani Zanzibar.