Azam Fc Yaiadhibu KmKm 2-0

Klabu ya Azam FC imejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMKM ya Zanzibar, katika mchezo wa kwanza wa hatua ya pili uliopigwa kwenye dimba la New Amaan Complex, Visiwani Zanzibar.
Azam FC, chini ya kocha Florent Ibenge, walionekana kuwa na ari kubwa tangu dakika za mwanzo za mchezo, wakitawala sehemu kubwa ya mchezo na kutumia vyema nafasi walizozipata. Bao la kwanza lilifungwa mapema dakika ya 6 kupitia kwa Jephte Kitambala aliyemalizia kwa ustadi pasi safi kutoka kwa Feisal Salum “Fei Toto”, akiipatia Azam FC uongozi wa mapema na kuwafanya mashabiki wa timu hiyo kushangilia kwa shangwe.
Licha ya KMKM kujaribu kurejea mchezoni, walijikuta wakipoteza umakini katika safu yao ya ulinzi na kuadhibiwa tena dakika ya 42, wakati Paschal Msindo alipoongeza bao la pili kwa shuti kali lililomshinda kipa wa KMKM bila majibu. Bao hilo liliwafanya vijana wa Chamazi kuingia mapumziko wakiwa kifua mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilishuhudia KMKM wakijaribu kurekebisha makosa yao kwa kufanya mabadiliko kadhaa, lakini walishindwa kupata bao la kufutia machozi kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Azam FC ikiongozwa na Yakub Mohamed na Edward Manyama. Kipa Daniel Akpeyi pia aliendelea kuwa imara kwa kuokoa michomo michache iliyolenga lango lake.
Kocha Florent Ibenge alipongeza nidhamu na umakini wa wachezaji wake baada ya mchezo, akisema kwamba bado hawajamaliza kazi kwani wanahitaji kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Oktoba 25 jijini Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Azam FC imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ikiwa ni mara ya kwanza baada ya misimu kadhaa. Mashabiki wa soka nchini Tanzania sasa wana matumaini kuwa wawakilishi hao wa nchi wataendelea kupeperusha vyema bendera ya taifa katika michuano hiyo ya kimataifa.

