Makonda Akutana Infantino Kujadili Maandalizi Afcon 2027

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Gianni Infantino, amesema wazi kuwa FIFA iko tayari kushirikiana kwa karibu na Tanzania katika programu mbalimbali za maendeleo zitakazolenga kukuza na kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu, hususan kwa kuwajengea vijana fursa za kunufaika na vipaji vyao kupitia michezo, elimu ya ufundi na ujenzi wa miundombinu bora.
Infantino ametoa kauli hiyo wakati wa kikao maalumu cha mazungumzo na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Paul Makonda, pembeni ya mechi ya fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 iliyochezwa jijini Rabat, Morocco. Mazungumzo hayo yalilenga kujadili mustakabali wa mpira wa miguu Tanzania na nafasi ya FIFA katika kuunga mkono maandalizi ya nchi kuelekea uenyeji wa AFCON 2027.

Akizungumza kwa msisitizo, Infantino aliipongeza Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikiwa katika sekta ya michezo, akieleza kuwa jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeanza kuzaa matunda, hasa katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya michezo ikiwemo viwanja, vituo vya mafunzo na mifumo ya maendeleo ya vijana.
“Tumeshuhudia dhamira ya dhati ya Serikali ya Tanzania katika kuwekeza kwenye michezo, hususan mpira wa miguu. FIFA iko tayari kushirikiana nanyi kikamilifu katika programu za maendeleo, kuanzia ngazi ya vijana hadi miundombinu na uendelezaji wa vituo vya ufundi vitakavyosaidia vijana kujiajiri na kujiendeleza kupitia michezo,” alisema Infantino.
Aliongeza kuwa uenyeji wa AFCON 2027 ni fursa adhimu kwa Tanzania kujitangaza kimataifa, si tu katika michezo bali pia kiuchumi, kijamii na kiutalii, huku FIFA ikiwa tayari kutoa ushirikiano wa kitaalamu, kiufundi na kimkakati ili kuhakikisha maandalizi yanafanyika kwa viwango vya juu vinavyokubalika kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri Paul Makonda alimshukuru Rais huyo wa FIFA kwa moyo wa ushirikiano anaouonesha kwa Tanzania, akisema kuwa Serikali inaona michezo kama nyenzo muhimu ya maendeleo ya vijana na taifa kwa ujumla. Makonda alisisitiza kuwa mpira wa miguu ni zaidi ya mchezo, bali ni ajira, afya, umoja na fursa ya kiuchumi kwa mamilioni ya Watanzania.
“Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaunga mkono kikamilifu maendeleo ya michezo na ametoa maelekezo ya wazi kuhakikisha Tanzania inajiandaa vyema kwa AFCON 2027. Serikali ipo tayari kushirikiana na FIFA katika kila hatua ili kuhakikisha ndoto hii inatimia kwa mafanikio makubwa,” alisema Makonda.
Makonda pia alitumia fursa hiyo kumkaribisha rasmi Gianni Infantino kuitembelea Tanzania, akisema ziara hiyo itampa fursa ya kujionea kwa macho yake maandalizi yanayoendelea kuelekea uenyeji wa AFCON, pamoja na miradi ya kimkakati ya michezo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Tanzania iko tayari kuwa mwenyeji wa matukio mbalimbali ya FIFA, ikiwemo mashindano ya kimataifa, mikutano ya viongozi wa soka duniani pamoja na ziara za wataalamu wa michezo. Tunaamini ushirikiano huu utafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya mpira wa miguu nchini,” aliongeza Makonda.

Mbali na hilo, Waziri huyo alieleza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha vipaji vya vijana vinatambuliwa mapema na kuendelezwa kwa misingi ya kitaalamu, kupitia akademi, ligi za vijana na programu za elimu zinazochanganya michezo na ufundi, ili kuwajengea mustakabali mpana hata baada ya maisha ya uchezaji.
Ushirikiano kati ya FIFA na Tanzania unatarajiwa kuimarisha zaidi juhudi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kusimamia na kuendeleza mchezo huo, huku wadau wa michezo wakitazamia kuona mageuzi makubwa katika miaka ijayo, hasa kuelekea AFCON 2027 itakayofanyika kwa pamoja Tanzania, Kenya na Uganda.
Kwa kauli ya Infantino na dhamira ya Serikali, matumaini ya soka la Tanzania kupiga hatua kubwa kimataifa yamezidi kuongezeka, huku macho ya mashabiki yakielekezwa kwenye utekelezaji wa ahadi hizi zitakazoweza kubadili taswira ya mpira wa miguu nchini na kuwapa vijana fursa mpya za kung’ara ndani na nje ya uwanja.
