Yanga Sc Yaanza Kwa Kishindo Caf

Yanga SC imeanza kampeni yake ya hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika kwa gia ya juu ya kibingwa, baada ya kuibuka na ushindi mwembamba lakini wenye thamani kubwa wa bao 1-0 dhidi ya FAR Rabat ya Morocco, mchezo uliochezwa kwenye dimba la Amaan Complex jijini Zanzibar.
Katika pambano hilo lililovuta hisia za maelfu ya mashabiki wa soka barani Afrika, Wananchi walionesha utulivu, nidhamu ya mchezo na mbinu za hali ya juu hasa eneo la kati lililokua na Duke Abuya,Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli huku wakitumia vyema nafasi chache walizozipata na hatimaye kuondoka na alama tatu muhimu.
Lakini stori kubwa zaidi ya usiku ilikuwa ni kurudi kwa mshambuliaji Prince Dube, aliyeonekana kama amefungua ukurasa mpya baada ya msururu wa michezo kupita bila kufumania nyavu msimu huu. Straika huyo kutoka Zimbabwe aliibuka kuwa shujaa wa Yanga baada ya kufunga bao pekee dakika ya 58, bao ambalo limeibua matumaini mapya kwa mashabiki na kumuongezea yeye kujiamini baada ya kipindi kigumu cha ukame wa mabao.
DUBE APIGA BAO LA KUJIAMINI, AMALIZA GUNDU
Bao hilo lilianza kwa kiungo Mzanzibari Mudathir Yahya ambaye aliweka pasi laini yenye makadirio mazuri, moja kwa moja kwa miguu ya Dube. Bila kusitasita, mshambuliaji huyo alikokota mpira kwa kasi iliyoacha mabeki wa FAR Rabat wakibaki wakitazamana, kisha kuachia shuti kali lisilozuilika lililokwenda kupasua nyavu na kuamsha vilio vya furaha kwenye Uwanja wa Amaan.
Wakati mashabiki wakishangilia, Dube alianguka chini akiwa amezungukwa na wachezaji wenzake, ishara ya nafuu ya kisaikolojia baada ya miezi ya presha na maneno mengi kutoka kwa mashabiki na wachambuzi wa soka. Bao lake halikuwa tu la ushindi bali ni ujumbe kwamba bado yupo na bado ana njaa ya mafanikio.
YANGA SC WALIPAMBANA KAMA FARASI WA VITA
Kipindi cha pili kilishuhudia Yanga wakiongeza kasi ya mashambulizi, wakitafuta bao la kuua mchezo mapema. Wakiwa mbele ya mashabiki wao, Wananchi walitawala sehemu ya kiungo kwa weledi mkubwa, huku Mudathir, Pacome na Maxi wakicheza kwa uelewano ulioifanya FAR Rabat kuonekana kama wamepoteza dira.
Mara kadhaa Yanga walikaribia kuongeza bao la pili kupitia Dube aliyekuwa akicheza kama mshambulizi huru lakini kipa wa FAR Rabat alifanya kazi ya ziada kuwatia matumaini wageni hao kutoka Morocco.
Kocha PabloConcalves, aliyekuwa akisimama pembeni ya uwanja kwa kujiamini kama daktari bingwa chumba cha upasuaji, alifanya mabadiliko ya kisayansi zaidi mwishoni mwa mchezo. Alimwingiza Lassine Kouma kuongeza nguvu katikati, Balla Moussa Conte kuongeza kasi eneo la namba 10, na Andy Boyeli kuleta nguvu mpya safu ya ushambuliaji. Mabadiliko hayo yalimsaidia Yanga kulinda ushindi na pia kutengeneza presha zaidi kwa FAR Rabat.
UJUMBE KWA AFRIKA: YANGA WANA NJAA YA MAFANIKIO

Ushindi huu umeipa Yanga mwanzo mzuri kwenye kundi gumu ambalo linajumuisha vigogo kadhaa wa Afrika. Lakini kama ilivyo kwa timu ya kiwango kikubwa, Wananchi hawajaweka kichwa chini; wanajua safari bado ni ndefu na kazi ipo mbele yao.
Kipenyo cha kuonesha uwezo wao kitafuata Ijumaa ijayo, Novemba 28, ambapo Yanga watapambana na JS Kabylie nchini Algeria, mchezo utakaopigwa saa 4 usiku kwa saa za Tanzania. Huu utakuwa mtihani mkubwa zaidi, mechi ya ugenini, baridi kali ya Kaskazini mwa Afrika, kelele za mashabiki wa nyumbanilakini pia fursa ya Yanga kujidhihirisha kwao na kwa bara zima kwamba safari yao msimu huu si ya bahati nasibu, bali ni ya maandalizi na ubora.
Mashabiki wa Yanga wana kila sababu ya kutabasamu, sio tu kwa ushindi huu, bali kwa namna timu ilivyocheza: utulivu, ubunifu, mbinu, na hamasa ya kupambana hadi dakika ya mwisho tofauti na ilivyokua chini ya kocha Roman Folz ambaye alitimuliwa klabuni hapo.



