Black Stars Yakubali Kipigo Algeria

Safari ya Singida Black Stars kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) imeanza kwa mtikisiko baada ya kukumbana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa CR Belouizdad ya Algeria, mchezo uliopigwa katika dimba la Nelson Mandela, Baraki. Vijana wa kocha Miguel Gamondi walionekana kukosa kasi, uthabiti na utulivu, hali iliyowapa wenyeji nafasi ya kutawala mchezo na kuutengeneza kwa ladha waliyoitaka tangu dakika za mwanzo kabisa.
Katika mchezo huo ambao CR Belouizdad walicheza kama wamezoea upepo wa kimataifa, Singida Black Stars waliingia wakionekana kuwa na hamasa lakini presha ya uwanja wa ugenini na kasi ya wapinzani wao iliwamaliza mapema.
Kocha wa Belouizdad, Sead Ramovic, alianza kwa kuisukuma timu yake mbele kwa kasi, jambo lililozalisha bao la mapema na kuiweka Singida kwenye hali ya sintofahamu iliyodumu kwa dakika zote 90.
BELHOCINI AFUNGUA SHEREHE, BENGUIT AKAMILISHA KIPIGO MAPEMA
Kabla mashabiki hawajakaa vizuri kwenye viti, dakika ya 5 Abdennour Belhocini alishafunga bao la kwanza kwa CR Belouizdad kwa kisigino huku Mabeki wa Singida walionekana kupoteana baada ya mpira kuchezwa kwa kasi, na kiungo huyo wa Belouizdad akapachika mpira wavuni kirahisi na kuamsha moto wa mashabiki wa wenyeji.
Dakika 14 tu zilipotimia, hali ikazidi kuwa mbaya kwa Singida Black Stars baada ya Abdelraouf Benguit kufunga bao la pili, akiunganisha mpira uliomkuta akiwa katika nafasi nzuri ndani ya boksi. Shuti lake lilikuwa safi, la utulivu na lisilompa kipa wa Singida nafasi ya kufanya chochote. Baada ya bao hilo, mchezo ulionekana kuwa wa upande mmoja, wenyeji wakimiliki mpira na kutengeneza nafasi wakati Singida wakijaribu kujituliza na kuokoa jahazi lililoanza kuzama mapema.
GAMONDI ACHANGANYIKWA, BLACK STARS WAPOTEZA MWELEKEO
Kwa sehemu kubwa ya mchezo, Singida walionekana wakijaribu kurejea mchezoni lakini ukuta wa Belouizdad haukuwa na nafasi ya huruma. Gamondi alifanya mabadiliko kadhaa kutafuta uhai lakini haikuzaa matunda. Viungo wake waliokuwa na majukumu ya kusambaza mipira walizuiwa vyema, huku washambuliaji wakikosa huduma yoyote ya maana kutoka katikati.
Presha ya mchezo, sauti za mashabiki na kasi ya wapinzani waliocheza kwa kujiamini kulifanya kikosi cha Singida kuonekana kama wageni wasiokuwa na ramani. Mpira haukukaa miguuni kwao muda mrefu, na hata walipopata nafasi ya kupandisha mashambulizi, walikosa maamuzi ya mwisho na uimara wa kupenya safu ya Belouizdad.
MAANDALIZI YA KUWAVAA STELLEBOCH YAANZA
Baada ya kipigo hicho cha kusikitisha, kikosi cha Singida Black Stars kimeanza kurejea nchini kwa mafungu mawili. Hatua hiyo imesababishwa na mipango ya safari pamoja na umuhimu wa kuanza mapema maandalizi ya mchezo wao wa pili wa hatua ya makundi dhidi ya Stelleboch FC ya Afrika Kusini, mchezo utakaopigwa wikiendi ijayo kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Habari kutoka ndani ya benchi la ufundi zinasema kuwa licha ya kipigo hicho, hali ya morali bado ni shwari. Wachezaji wameelezwa kuchukulia matokeo hayo kama somo, huku Gamondi akiahidi kufanya marekebisho makubwa, hasa katika safu ya ulinzi na eneo la kiungo ambalo lilionekana kupwaya sana dhidi ya Belouizdad.
Wachezaji wanaorejea mapema wanatarajiwa kuanza mazoezi jijini Zanzibar mara tu watakapowasili, wakilenga kurejesha kasi, kujiamini na kuunganisha nguvu mpya kabla ya kukutana na Stelleboch ambao nao hawatakuwa wageni wa mchezo mgumu.
KUSHAMBULIA MWANZO MWISHO AMAAN
Mchezo dhidi ya Stelleboch FC unatarajiwa kuwa vita ya uhai ndani ya kundi lao. Singida wakipoteza tena, safari yao ya CAFCC inaweza kuingia kwenye hatari kubwa. Lakini wakishinda, watarejesha matumaini na kuonesha kuwa bado wana nafasi ya kupambana na vigogo wa kundi hilo.
Mashabiki wa Singida Black Stars sasa wanatazama Amaan kwa matumaini, wakiwa na imani kuwa nyumbani kutawapa nguvu ya ziada. Ni wakati wa Gamondi na vijana wake kupambana, kuonyesha ubora wao na kuweka rekodi mpya katika historia ya klabu.



