Azam Fc Yakubali Kipigo Caf

587356040 18539847337052678 3903360173159057902 n

Azam FC wameanza kwa mtikisiko safari yao ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) baada ya kukumbana na kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa AS Maniema Union kwenye Uwanja wa Stade des Martyrs, Kinshasa,Licha ya matarajio na matumaini waliyokuwa nayo kabla ya mchezo, kikosi cha Chamazi kilionekana kulegalega katika maeneo muhimu na kushindwa kutumia fursa chache walizopata.

Kocha wa AS Maniema Union, mkongwe wa soka la Afrika Papy Kimoto, alionyesha kwa nini anaheshimika barani. Mbinu zake, uzoefu wake, pamoja na ubora wa wachezaji wake wa kimataifa ziliifanya Maniema kuonekana timamu, imara na hatari kila walipotengeneza shambulizi. Wakati huo huo, Azam waliingia uwanjani wakiwa na imani ya kuiba angalau pointi moja ugenini, lakini kutokuwa na ukakamavu kwenye maamuzi ya mwisho kuliumiza juhudi zao.

583953700 18539845678052678 236501418691795803 n

KIPINDI CHA KWANZA: WOTE WABANA, MANIEMA WANAPATA ZAWADI YA MAKOSA

Kwa dakika nyingi za kipindi cha kwanza, mchezo ulikuwa wa kukabana na kushikana. Ibenge aliweka mfumo wa kupiga pasi kwa utulivu na kasi ya kushtukiza, huku Azam wakijaribu kutawala eneo la katikati kupitia Feisal Salum na Yahaya Zayd huku
Jephte Kitambala aliyerejea kukutana na timu yake ya zamani alikuwa akitafuta nafasi za kuumiza lakini safu ya ulinzi ya Maniema ilimzuia mara zote, ikiongozwa na nahodha wao jasiri Osee Ndombele.

Hata hivyo, mambo yakabadilika dakika chache kabla ya halftime. Uzembe kwenye eneo la ulinzi la Azam Fc uliwapa wenyeji nafasi ya kuiba mpira na M-Burkinabe fundi wa mpira, Clément Pitroipa, aliutwaa mpira na kutoa pasi tamu kama asali kwa Christian Balako, ambaye alimalizia bila presha ndani ya boksi. Bao hilo lilikuwa pigo kwa Azam ambao hadi muda huo walikuwa wakihimili mashambulizi.

KIPINDI CHA PILI: MANIEMA WAFUNGA MILANGO, AZAM WASHINDWA KUPASUA

Baada ya kurudi kutoka mapumziko, Maniema Union hawakuwa na haraka ya kushambulia. Walipunguza kasi, wakakubali kumiliki mpira kidogo huku wakiegemea zaidi kwenye ukuta wao imara ulioongozwa na Ndombele.
Azam walijaribu kutafuta bao la kusawazisha kupitia Feisal ‘Fei Toto’ ambaye alionekana kuwa injini ya timu, lakini mipira yake ilizuiwa ama ilikosa malengo. Kitambala, licha ya nguvu na kasi, hakuweza kupenya ngome ya Maniema ambayo ilikuwa imesimama imara kama ukuta wa Berlin.

583953700 18539845678052678 236501418691795803 n 1

Kwa muda mwingi, mashambulizi ya Azam yalikuwa ni kama makosa yaliyopangwa hakuwa na ufanisi, hakuna maamuzi ya mwisho, hakuna shuti lililoleta hofu ya kweli kwa wenyeji. Hii iliwapa wenyeji nafasi ya kutulia na kuutafuta muda sahihi wa kupeleka pigo la mwisho.

Dakika ya 85, ndoto za Azam kupata angalau pointi moja zikayeyuka rasmi. Shambulizi maridadi kutoka upinde wa kulia lilizaa matunda baada ya mchezaji wa akiba Sylva Tshitenge kutoa krosi ya kiwango cha juu, ambayo ilikutana kichwa cha Chadoma Ozome. Kipa wa Azam Fc Zubeir Foba hakuwa na cha kufanya mpira ulitinga nyavuni na kuwaweka wenyeji mbele 2-0.

Bao hilo lilizima kabisa juhudi za Azam ambao hadi mwisho wa mchezo walionekana kuchoka, kuchanganyikiwa na kukosa mbinu ya kupenya ukuta wa Maniema ambao ulikuwa kikwazo cha wazi.

TASWIRA YA KIKOSI: AZAM WANATOKA WAMEJIKUNA, MANIEMA WANATOKA KIBABE

Kwa kiwango walichokionesha, Azam Fc lazima wajilaumu. Walicheza kwa kujilinda zaidi badala ya kushambulia kama wanavyofanya nyumbani. Safu yao ya kiungo haikutoa ubunifu wa kutosha, na washambuliaji walidhibitiwa kwa urahisi mno huku kwa upande wa Maniema, ushindi huu ni ishara wazi kuwa wao si wageni wa bahati ni timu iliyojengwa, yenye nidhamu na mbinu safi.

ANGALIA HATUA INAYOFUATA NI NGUMU ZAIDI

AS Maniema Union wataingia uwanjani tena Jumapili ijayo wakisafiri kwenda Kenya kukipiga na Nairobi United, wakitafuta kuendeleza mwanzo wao mzuri wa Kundi B.

Kwa upande wa Azam, mambo ni moto zaidi. Watarudi Chamazi kukabiliana na Wydad AC ya Morocco miongoni mwa wababe wakubwa wa Afrika. Lazima washinde ili kurejesha matumaini yao ya kusonga mbele. Kosa lolote litakuwa kama tunda lililoiva, litakalovutwa na mvuto wa ardhi.

Mashabiki wao wanategemea kuona Azam mpya inayocheza kwa ujasiri, kasi, mipango, na umakini wa hali ya juu,Kwa sasa, Azam wanabeba mzigo mzito, Maniema wanashangilia, na Kundi B linawaka moto kutokana na msimamo ulivyo mpaka sasa.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks