Stars Yawakosa Feitoto,Yakub Dhidi ya Nigeria

Kikosi cha Tanzania ‘Taifa Stars’ kimeingia kwenye mtihani mzito kabla ya mchezo wake muhimu wa hatua ya makundi ya AFCON 2025 dhidi ya Nigeria, baada ya kuthibitika kuwa wachezaji watatu muhimu hawatakuwepo kwenye pambano hilo litakalochezwa leo Desemba 23 saa 2:30 usiku.
Wachezaji hao ni Selemani Mwalimu, Yakoub Suleman na Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambao kwa pamoja wameacha pengo kubwa kwenye kikosi cha kocha mkuu Miguel Gamondi. Mwalimu na Yakoub ni majeruhi, huku Feisal akilikosa pambano hilo kutokana na adhabu ya kadi mbili za njano.

Taarifa za kumkosa beki Yakoub Suleman kwenye mechi zote za hatua ya makundi zimepokelewa kwa maumivu makubwa ndani ya kambi ya Taifa Stars, kwani ni miongoni mwa wachezaji waliokuwa wanategemewa kuimarisha safu ya ulinzi dhidi ya vigogo wa Afrika.
Pigo Kubwa Lango la Taifa Stars
Mbali na changamoto hizo, lango la Taifa Stars limeingia kwenye sintofahamu kubwa baada ya kuonekana wazi kuwa chaguo la makipa limekuwa finyu zaidi. Kwa sasa, waliosalia ni Hussein Masalanga, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akikalia benchi klabuni Singida Black Stars, na Zuberi Foba, golikipa kijana anayekuja kwa kasi lakini bado hana uzoefu mkubwa wa mashindano makubwa ya kimataifa.

Hali hiyo inamlazimisha Gamondi kuchukua uamuzi mgumu na wa hatari, kati ya kumwamini Masalanga ambaye hana ‘match fitness’ ya kutosha, au kumtupa kwenye moto Foba ambaye ni junior na bado anahitaji kuvumiliwa kwenye makosa ya kiasili ya umri wake.
Kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na benchi la ufundi, Gamondi amekuwa akifanya tathmini ya mwisho hadi dakika za mwisho kabla ya mchezo, akitambua kuwa makosa madogo dhidi ya Nigeria yanaweza kugharimu timu matokeo mabaya na Foba ndiye ambaye amepangwa kuanza langoni.
Nigeria Ni Mtihani Mwingine
Taifa Stars inakwenda kuivaa Nigeria ikijua wazi kuwa inakutana na moja ya timu zenye uzoefu mkubwa barani Afrika, yenye wachezaji wanaocheza ligi kubwa Ulaya. Hata hivyo, Gamondi amesisitiza mara kadhaa kuwa timu yake haina sababu ya kuogopa, bali inapaswa kucheza kwa nidhamu, umakini na ujasiri.
Mashabiki wa soka nchini wanatarajia kuona mabadiliko ya kiufundi, hasa katika eneo la kiungo baada ya kukosekana kwa Feisal Salum, ambaye mchango wake katika kusukuma mashambulizi na kupiga pasi za mwisho umekuwa muhimu kwa Taifa Stars.
Waamuzi Watangazwa Rasmi
Wakati presha ya mchezo ikiendelea kupanda, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetangaza rasmi waamuzi wa pambano hilo. Mwamuzi wa kati atakuwa Dahane Beida kutoka Mauritania, mwamuzi mwenye uzoefu mkubwa katika mashindano ya CAF na FIFA.
Atasaidiwa na:
- Jerson Emiliano (Angola) – Mwamuzi msaidizi wa kwanza
- Ivanildo (Angola) – Mwamuzi msaidizi wa pili
- Clement Franklin (Ivory Coast) – Mwamuzi wa nne
Katika teknolojia ya VAR, atakuwepo:
- Haggag Hussam (Misri) – VAR
- Abdulrazg Ahmed (Libya) – Msaidizi wa VAR
Wakati tathmini ya waamuzi itasimamiwa na Lidya Tafesse kutoka Ethiopia, mmoja wa wakaguzi wenye heshima kubwa barani Afrika.
Moyo wa Mapambano
Licha ya changamoto zote, kambi ya Taifa Stars inaamini bado ina nafasi ya kufanya vizuri ikiwa wachezaji waliopo watatimiza majukumu yao kwa nidhamu na kujituma. Gamondi amesisitiza kuwa AFCON ni mashindano ya mshikamano na kupambana, si majina makubwa pekee.
Mchezo wa leo dhidi ya Nigeria utaonyesha kama Taifa Stars itaweza kuvuka mawimbi ya majeraha, adhabu na presha ya mashabiki, au kama changamoto hizo zitakuwa mzigo mzito katika safari yao ya AFCON 2025.

