Stars Yapigwa na Nigeria Afcon

b25lwnr2301

Safari ya timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars” kwenye michuano ya TotalEnergies Afcon Morocco 2025 imeanza kwa maumivu, baada ya kupoteza kwa bao 2–1 dhidi ya Nigeria katika mchezo uliochezwa Jumanne jioni, huku nyota Ademola Lookman akifunga bao la ushindi dakika chache tu baada ya Tanzania kusawazisha.

Nigeria, maarufu kama Super Eagles, ilionekana kutawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza, ikionesha uzoefu na ubora wa wachezaji wake wanaocheza soka la kiwango cha juu barani Ulaya ambapo shinikizo lao lilizaa matunda dakika ya 36, pale beki Semi Ajayi alipopanda juu zaidi na kupiga kichwa safi kilichomalizia mpira wavuni, akitumia kona iliyopigwa na Alex Iwobi.

Kona hiyo ilipatikana muda mfupi baada ya beki wa Taifa Stars, Bakari Mwamnyeto, kuokoa hatari kubwa kwa kuondoa mpira uliokuwa tayari unaelekea wavuni baada ya shuti la karibu la Victor Osimhen. Tukio hilo lilionesha namna ambavyo Nigeria ilianza kuongeza kasi na kuamini inaweza kuifunga Tanzania.

Presha Kubwa ya Nigeria, Nidhamu ya Tanzania

Kwa kipindi cha kwanza, Osimhen, Lookman na Moses Simon waliisumbua safu ya ulinzi ya Taifa Stars kwa kasi, mipango ya kubadilishana nafasi na mbinu za kushambulia kwa kushtukiza. Licha ya presha hiyo, Tanzania ilisimama imara kwa nidhamu ya hali ya juu, ikiruhusu bao moja tu kabla ya mapumziko.

Nigeria ilishindwa kuongeza bao la pili licha ya kumiliki mpira kwa muda mrefu, hali iliyowapa Taifa Stars matumaini ya kurejea vizuri kipindi cha pili.

Kipindi cha Pili Chawaka Moto

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi isiyo ya kawaida. Ndani ya dakika ya kwanza tu, Nigeria ilidhani imeongeza bao la pili baada ya Osimhen kuingiza mpira wavuni kwa kisigino, lakini baada ya VAR kuhusika, bao hilo lilifutwa kwa madai ya kuotea.

Total Energies AFCON 2025 50 Nigeria 🇳🇬 1️⃣ 1️⃣ 🇹🇿@TaifaStars charles ⚽️ @taifastars @n

Uamuzi huo uliipa Tanzania nguvu mpya. Dakika chache baadaye, kiungo Novatus Dismas alipiga pasi ya chonganishi iliyochana kabisa safu ya ulinzi ya Nigeria, ikimkuta Charles M’mombwa aliyechangamka kwa kasi na kumalizia kwa utulivu, akimpita golikipa Stanley Nwabali na kusawazisha bao hilo.

Uwanja ulilipuka kwa shangwe, mashabiki wa Tanzania wakiamini huenda historia ikaandikwa.

Lookman Aua Ndoto za Taifa Stars

Hata hivyo, furaha hiyo haikudumu. Ndani ya sekunde 60 tu, Ademola Lookman alionesha ubora wa hali ya juu, akipokea mpira nje kidogo ya eneo la hatari na kupiga shuti lililopinda kwa ustadi mkubwa, mpira uliomshinda golikipa wa Tanzania Zubeiry Foba na kuingia wavuni bila huruma.

Total Energies AFCON 2025 55 Nigeria 🇳🇬 2️⃣ 1️⃣ 🇹🇿@TaifaStars charles ⚽️ @taifastars @n

Bao hilo lilizima kabisa shangwe za Taifa Stars na kurejesha utulivu kwa Nigeria, ambao kuanzia hapo walicheza kwa uzoefu mkubwa, wakimiliki mpira na kupunguza hatari langoni mwao.

Taifa Stars Yasukuma Mpaka Mwisho

Licha ya kurudi nyuma, Taifa Stars haikukata tamaa. Ilisukuma mashambulizi ikitafuta bao la kusawazisha, na ilikaribia kupata nafasi hiyo katika dakika za mwisho baada ya Ibrahim Hamad kupiga shuti akimalizia mpira wa kona, lakini mpira ulipita pembeni mwa lango.

Nigeria ilisimama imara hadi filimbi ya mwisho, ikihakikisha inaondoka na pointi tatu muhimu katika mchezo wa ufunguzi.

Kauli za Makocha na Nyota wa Mechi

Mfungaji wa bao la kwanza, Semi Ajayi, alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi ambapo alisema kuwa
“Ni hisia nzuri sana kufunga kwa ajili ya nchi yangu, hasa katika mchezo kama huu. Tulifanya vizuri AFCON iliyopita Ivory Coast na tunaitumia kama kipimo chetu. Sisi si timu ya kutegemea washambuliaji pekee kufunga mabao, na inafurahisha kuchangia mafanikio ya timu.”

Naye Kocha wa Nigeria, Eric Chelle, alisema “Tumefurahia pointi tatu, hilo ndilo jambo muhimu zaidi. Kipindi cha pili kimeonesha bado tuna kazi ya kufanya, hasa namna ya kuua mechi mapema. Tunatambua hilo na tutafanyia kazi.”

Kwa upande wa Tanzania, kocha Miguel Ángel Gamondi alijivunia kikosi chake akisema “Nadhani Tanzania imecheza vizuri kuliko wengi walivyotarajia. Nigeria ilikuwa na umiliki mkubwa wa mpira, lakini tuliwadhibiti vizuri kupitia mfumo wetu wa kiufundi. Nafikiri tumewashangaza watu wengi kwa kiwango chetu.”

Matarajio Yabaki Hai

Ingawa Taifa Stars imeanza kwa kipigo, kiwango walichoonesha dhidi ya moja ya vigogo wa Afrika kimeacha matumaini makubwa kwa mashabiki wa soka nchini. Ikiwa wataendelea kucheza kwa nidhamu, ujasiri na kujiamini, Tanzania bado ina nafasi ya kupambana katika michezo ijayo ya kundi.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks