Zimbabwe Yakubali Kipigo Jioniii

Kazi imeanza rasmi! Ndio, pazia la Kundi B la michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) lilianza kwa vishindo Jumatatu iliyopita, pale Mashetani Wekundu wa Misri walipolazimika kutumia akili ya ziada kuwachapa wapinzani wao shupavu, Zimbabwe, kwa ushindi mwembamba wa 2-1 katika Mtanange uliopigwa kwenye Uwanja wa Stade Adrar, Agadir,
Mchezo huo ulikuwa ni wa presha ya juu kuanzia mwanzo hadi mwisho, na kuthibitisha kuwa hakuna tena ‘vibonde’ kwenye soka la Afrika.
Dube Awainua Wazimbabwe Mapema
Misri, chini ya kocha wake mkuu Hosam Hassan,ilitarajiwa kuingia uwanjani na kumaliza kazi mapema kutokana na ubora wa kikosi chake kilichosheheni nyota wanaocheza Ulaya. Lakini, harakati zao zilianza kusuasua kwani Zimbabwe, ‘The Warriors’, walionekana kuja na mbinu moja tu: kufa na kupona wakijazana katikati na kufanya shambulizi la kushtukiza ambalo liliacha mashabiki wa Misri midomo wazi.

Ilikuwa ni dakika ya 20 pekee, beki wa Misri alifanya makosa ya kitoto yaliyoashiria baada ya kujichanganya kwa miguu, na mshambuliaji matata wa Zimbabwe, Prince Dube, hakufanya ajizi. Alipiga shuti la chinichini lililompita kipa wa Misri na kujaa wavuni na kuufanya Uwanja kupigwa na ukimya wa ghafla, isipokuwa kelele za mashabiki wachache wa Zimbabwe. Ilionekana kama historia mpya inaandikwa Agadir.
Salah Apotea, Marmoush Afufua Matumaini
Kipindi cha kwanza kilimalizika huku Misri ikiwa nyuma, jambo ambalo liliongeza presha kwa wachezaji na benchi la ufundi. Nyota wao mkuu, Mohamed Salah, alikuwa akijaribu kila mbinu lakini alikabwa kiasi cha kupoteza kabisa uwezo wake wa kupenya. Zimbabwe walikuwa wamejipanga, wakiacha pengo dogo sana kwa Misri kutumia.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi mpya. Misri walifanya mabadiliko kadhaa na kuanza kulisakama lango la Zimbabwe kama nyuki. Dakika ya 64, ndipo nuru ilipoonekana tena. Winga fundi Omar Marmoush alipata mpira nje kidogo ya eneo la hatari, akasogea hatua mbili na kupiga mkwaju mkali wa mguu wa kushoto ambao ulitingisha wavu. Golikipa wa Zimbabwe alijitupa lakini mpira ulikuwa umeshaingia na kufanya ubao kusomeka 1-1 Mlipuko wa shangwe ulionekana kuamsha tena uwanja.
Zahama Dakika za Mwisho, Shujaa Ajitokeza
Mchezo ulikuwa sasa ni moto wa kuotea mbali. Kila timu ilitaka ushindi. Zimbabwe hawakurudi nyuma, walijaribu mashambulizi ya kushtukiza huku Misri wakisaka goli la ushindi kwa udi na uvumba. Muda wa kawaida ulimalizika na mwamuzi aliongeza dakika tano za majeruhi.

Hapo ndipo soka lilionyesha maajabu yake. Ilikuwa ni dakika ya 90 na sekunde chache mbele (90+1), Misri walipata kona. Mpira ulipigwa na kuokolewa na mabeki wa Zimbabwe, lakini ulimfikia yule yule anayezoeleka kwa nyakati ngumu, mchezaji bora wa Afrika mara kadhaa, Mohamed Salah.
Salah alipokea mpira, akawazidi ujanja mabeki wawili na kupiga shuti la taratibu lakini lenye akili nyingi lililotinga wavuni. 2-1 Mchezaji huyo wa Liverpool alilipuka kwa shangwe, wachezaji wenzake wakamrukia, na uwanja mzima wa Agadir ukawa kama umeme umepita. Kilio cha furaha kilitawala huku ndoto za Zimbabwe zikizimika papo hapo.
Mwamuzi alipuliza filimbi ya mwisho muda mfupi baada ya goli hilo. Misri ikapata alama zote tatu muhimu katika safari yao ya kusaka ubingwa wa 8 wa AFCON.
Msimamo wa Kundi B
Ushindi huu unaifanya Misri kukaa kileleni mwa Kundi B, wakiwa na pointi 3 sawa na Afrika Kusini ambao nao walishinda mchezo wao wa kwanza. Zimbabwe wamebaki mkiani bila alama.
Kwa mtindo huu, Kundi B linatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, na kila mchezo utakuwa fainali. Mashabiki wanatarajia burudani zaidi kutoka kwa vigogo hawa. Mechi ijayo kwa Misri itakuwa ni mtihani mwingine mzito, na macho yote yatakuwa kwa Salah tena

