Tunisia Yaanza AFCON 2025 kwa Kishindo, Yaifunga Uganda 3–1 Rabat

نهاية المباراة 🔚إنتصار مهم و أداء جيد لمنتخبنا الوطني التونسي أمام نظيره الأوغندي بنتيجة 3 1

Timu ya taifa ya Tunisia, maarufu kama Carthage Eagles, imeanza vyema safari yake ya michuano ya TotalEnergies CAF AFCON Morocco 2025 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 3–1 dhidi ya Uganda katika mchezo uliochezwa Jumanne jioni kwenye Uwanja wa Annex Olympic, uliopo ndani ya Prince Moulay Abdellah Sports Complex mjini Rabat.

Kwa kuonesha soka la nidhamu, kasi na mpangilio mzuri wa kiufundi, Tunisia ilitawala mchezo huo kuanzia dakika za mwanzo hadi mwisho, ikiashiria mapema dhamira yake ya kufanya vizuri katika mashindano hayo ya bara.

Tunisia Yaanza kwa Kasi

Tunisia ilichukua udhibiti wa mchezo mapema na haikuchukua muda mrefu kupata bao la kuongoza. Dakika ya 10, Elyes Skhiri aliwafurahisha mashabiki baada ya kumalizia kwa shuti la uhakika mpira wa kugongeana kwa pasi nyingi ulioshirikisha wachezaji kadhaa, bao lililoonesha kiwango cha juu cha uelewano wa timu hiyo.

b25lwwm0225b
Montassar Omar Talbi of Tunisia during the 2025 Africa Cup of Nations AFCON match between Tunisia and Uganda at Olympique Stadium in Rabat, Morocco on 23 December 2025 ©Weam Mostafa\BackpagePix

Baada ya bao hilo, Carthage Eagles waliendelea kushambulia kwa mpangilio mzuri, wakitawala umiliki wa mpira huku Uganda ikionekana kushindwa kuhimili kasi na presha ya wapinzani wao.

Achouri Aendelea Kuua Ndoto za Uganda

Dakika chache kabla ya mapumziko, Tunisia iliongeza bao la pili kupitia Mohamed Elyes Achouri, ambaye alionesha utulivu mkubwa ndani ya eneo la hatari na kufunga bao safi dakika ya 40. Bao hilo lilizidisha ugumu kwa Uganda, waliokwenda mapumzikoni wakiwa nyuma kwa mabao mawili kwa bila.

Uganda ilijaribu kupambana, lakini ilishindwa kushinda mipambano ya kati ya uwanja, hali iliyowaacha wakilazimika kujilinda kwa muda mrefu.

Kipindi cha Pili, Tunisia Yadhibiti Mechi

Baada ya mapumziko, kikosi cha kocha Sami Trabelsi kiliendelea kuonesha ukomavu wa hali ya juu. Wachezaji wake walibaki imara, wakicheza kwa umakini mkubwa na kuzuia hatari zozote kuelekea lango lao.

The second half is underwayTunisia 2 0 UgandaTotalEnergiesAFCON2025

Dakika ya 64, Achouri alikamilisha bao lake la pili baada ya kumalizia kwa ustadi shambulizi la haraka, na kuifanya Tunisia kuongoza kwa mabao 3–0, hali iliyowafanya mashabiki wengi wa Uganda kuanza kukata tamaa.

Uganda Yapata Bao la Kufutia Machozi

Licha ya kuwa nyuma kwa mabao matatu, Uganda haikukata tamaa kabisa. Katika dakika za nyongeza, Denis Omedi alitumia uzembe mdogo wa safu ya ulinzi ya Tunisia na kufunga bao la kufutia machozi, lakini bao hilo halikubadilisha hatima ya mchezo huo.

Tunisia ilisimamia vyema dakika za mwisho na kuhakikisha inaondoka na pointi tatu muhimu.

Kauli za Makocha

Kocha wa Uganda, Paul Put, alikiri wazi kuwa timu yake ilianza vibaya na ilionesha heshima kubwa kupita kiasi kwa Tunisia.

“Tuliwaogopa sana. Tunajua wao ni wazuri kwenye mipira ya adhabu. Huu ni mwanzo mbaya. Hatukuwa wakali vya kutosha. Ukicheza AFCON, lazima ushinde mipambano. Tulicheza vizuri kwa dakika 25 tu, muda uliobaki tulikuwa tunajilinda, na hiyo haitoshi kwa mashindano kama haya,” alisema Put.

Kocha huyo aliongeza kuwa sasa Uganda italazimika kucheza michezo ijayo chini ya presha kubwa, akisisitiza kuwa sare haitoshi tena, bali ushindi ndio chaguo pekee ili kuendelea kuwa na matumaini ya kusonga mbele.

Kwa upande wa Tunisia, kocha Sami Trabelsi alieleza kuridhishwa kwake na kiwango cha wachezaji wake, akibainisha kuwa baadhi yao walicheza zaidi ya matarajio.

“Tulikuwa na wachezaji wengine waliofanya vizuri kuliko tulivyotarajia. Timu kwa ujumla ilikuwa imara sana. Lengo letu ni kuboresha kiwango chetu kila mechi tunapopata mwendelezo,” alisema Trabelsi.

Alisifu pia maandalizi ya waandaaji wa mashindano, akisema licha ya mvua kubwa kunyesha, uwanja uliendelea kuwa katika hali nzuri na inayoruhusu soka la kiwango bora kuchezwa.

Achouri Atoa Shukrani

Mfungaji wa mabao mawili, Mohamed Elyes Achouri, aliwapongeza wachezaji wenzake na mashabiki waliijitokeza kwa wingi licha ya hali ya hewa kuwa mbaya.

“Nawashukuru wachezaji wenzangu kwa kazi kubwa waliyofanya. Pia nawapongeza mashabiki waliokuja kwa wingi kwenye mvua. Tunatumaini tumewafanya wajivunie,” alisema Achouri.

Mwanzo Mzuri kwa Tunisia

Kwa ushindi huu, Tunisia imeanza kampeni yake ya Kundi C kwa hatua madhubuti, ikionesha kuwa ni miongoni mwa timu zinazokuja kwa malengo makubwa AFCON 2025. Kwa Uganda, kazi bado ni nzito, lakini bado wana nafasi ya kurekebisha makosa yao katika michezo ijayo.

Leave a Reply

Enable Notifications OK No thanks