Diallo Aiongoza Ivory Coast Robo Fainali, Burkina Faso Yalazwa 3-0

Safari ya Côte d’Ivoire (Ivory Coast) katika harakati za kulitetea taji la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Morocco 2025 imeendelea kushika kasi, baada ya mabingwa watetezi hao kuichapa Burkina Faso mabao 3-0 na kufuzu kwa kishindo hatua ya robo fainali.
Katika mchezo huo uliochezwa usiku wa Jumanne jijini Marrakesh, nyota wa Manchester United, Amad Diallo, aliibuka tena kuwa mhimili wa mafanikio ya Tembo wa Afrika Magharibi, akifunga bao la kwanza na kutoa pasi ya bao la pili, akionyesha wazi kuwa ubora wake unaongezeka kadri mashindano yanavyoendelea.
Ushindi huo sasa umeiweka Ivory Coast kwenye mchuano mkubwa wa robo fainali dhidi ya Misri, mabingwa wa kihistoria wa AFCON, katika mechi inayotarajiwa kuchezwa Jumamosi mjini Agadir, pambano linalotabiriwa kuwa moto wa kuotea mbali.


Ivory Coast ilianza mchezo kwa kasi ya hali ya juu, ikiwabana Burkina Faso tangu dakika za mwanzo. Wachezaji wa pembeni Amad Diallo na Yan Diomandé walikuwa tishio la kudumu, wakitumia kasi, mbio na mizunguko ya haraka kuipasua safu ya ulinzi ya Burkinabè.
Mashambulizi ya Ivory Coast yalikuwa yakikatiza kila kona ya uwanja, huku Burkina Faso wakijikuta wakilazimika kurudi nyuma na kujilinda kwa muda mrefu. Shinikizo hilo hatimaye lilizaa matunda katika dakika ya 20, baada ya makosa madogo ya mawasiliano kati ya mabeki wa Burkina Faso ndani ya eneo la hatari.
Mpira ulipigana kwa muda mfupi kati ya mabeki hao wawili, ndipo Diallo akaibukia ndani ya boksi, akauchukua mpira kwa utulivu mkubwa na kumpiga chenga ndogo kipa kwa kuuchopu mpira juu, bao lililowafanya mashabiki wa Ivory Coast kulipuka kwa shangwe.
Dakika 12 baadaye, Diallo alibadilika kutoka mfungaji hadi mtoa pasi. Akiwa pembeni, alipiga krosi ya chini yenye macho mbele ya lango, ambapo Yan Diomandé aliupokea kwa mguso wa kwanza wa utulivu kabla ya kupiga shuti kali la chini lililompita kipa na kuifanya Ivory Coast iongoze kwa mabao 2-0.
Burkina Faso walijaribu kurejea mchezoni kabla ya mapumziko, na walikuwa karibu kupunguza tofauti ya mabao pale Dango Ouattara alipokimbia kwa kasi upande wa kulia na kupiga shuti la chini, lakini mpira huo uligonga mwamba wa lango (posti) na kurejea mikononi mwa kipa wa Ivory Coast, hali iliyowakatisha tamaa mashabiki wa Stallions.

Kipindi cha pili kilianza kwa sura tofauti, Burkina Faso wakionekana kurejea wakiwa na ari mpya. Waliongeza mashambulizi na kujaribu kuibana Ivory Coast kwa muda mrefu, wakitafuta bao la mapema litakalowarudisha kwenye mchezo.
Hata hivyo, walikuta ukuta mgumu wa safu ya ulinzi ya Ivory Coast, iliyoongozwa kwa nidhamu, umakini na utulivu mkubwa. Mabeki wa Ivory Coast walikuwa wakisoma mchezo vizuri, wakikatiza pasi, kushinda mipambano ya ana kwa ana na kurejesha mpira haraka kila ulipopotea.
Kadri dakika zilivyosonga, matumaini ya Burkina Faso yalizidi kufifia, na pigo la mwisho lilikuja dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho. Ivory Coast walivamia kwa shambulizi la kushtukiza, ambapo Odilon Kossounou alimtumia pasi ya uhakika Ousmane Diomandé, naye hakufanya makosa, akipiga shuti la karibu lililotinga wavuni na kuhitimisha ushindi wa mabao 3-0.
Baada ya bao hilo, Ivory Coast walitawala mchezo kwa utulivu, wakimiliki mpira na kuua dakika za mwisho bila presha, kabla ya filimbi ya mwisho kuthibitisha ushindi wao mnono na tiketi ya robo fainali.
Kauli za Makocha Baada ya Mchezo
Amad Diallo Mchezaji Bora wa Mechi alisema kuwa “Kikubwa ni kwamba tulipambana kama timu. Kila mchezaji yupo tayari kuchangia kwa namna yoyote. Kuna mshikamano mkubwa uwanjani, kuna maelewano yanayofanya mchezo wetu utembee kwa urahisi. Hakuna anayetaka kuwa shujaa peke yake. Nikiona mwenzangu yupo kwenye nafasi nzuri, namchezea mpira. Hivyo ndivyo tunavyocheza,” alisema Diallo.
Huku Brama Traoré Kocha Mkuu, Burkina Faso alisisitiza kuwa kuwakosa wachezaji wake muhimu ilikua ni sababu kubwa ya wao kupoteza mchezo huo “Kwa bahati mbaya mambo hayakwenda sawa kwetu. Tulikuwa na upungufu wa wachezaji muhimu, na hilo lilionekana wazi. Kukosa wachezaji watatu wa msingi kunakuathiri sana. Kiufundi hatukuwa bora, mfumo tuliouandaa haukufanya kazi, na mimi nachukua dhamana ya hilo,” alisema Traoré.
Emerse Faé Kocha Mkuu, Ivory Coast alisema kuwa ushindi huo ni matokeo ya ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja kama timu “Nilivutiwa sana na namna tulivyorejea haraka pale tulipopoteza mpira. Kila tulipopoteza umiliki, wachezaji walijibu mara moja. Kulikuwa na presha, lakini walijituma kurejesha mpira kwa haraka. Tulishinda mipambano mingi, tukakata pasi nyingi. Kilichonifurahisha zaidi ni kwamba haikuwa jitihada ya mtu mmoja, bali nguvu ya timu nzima,” alisema Faé.
Kwa ushindi huu, Ivory Coast wanaendelea kuthibitisha kuwa ubingwa wao wa AFCON walioupata nyumbani haukuwa wa bahati, huku macho sasa yakielekezwa kwenye pambano kali dhidi ya Misri, mchezo utakaopima kwa undani ndoto yao ya kubeba taji la pili mfululizo.

